AFISA Elimu Mkoa wa Mbeya, Juma Kaponda
amewaagiza Wakuu wa Shule za Sekondari, Waratibu Elimu Kata na Maafisa Michezo
kuhakikisha hawajumuishi wanafunzi wa kidato cha nne katika kushiriki
mashindano ya Umiseta.
Alisema mashindano yatakayofanyika Mwakani
yasiwahusishe wanafunzi wa kidato cha Nne kutokana na kuwa ni darasa la
mitihani ya Taifa hivyo kuwafanya kukosa maandalizi ya kutosha pindi wanapokuwa
wamechaguliwa kushiriki michezo hiyo ambayo hufanyika katika kituo kimoja
ambacho ni mbali na shule zao.
Maagizo hayo aliyatoa mwishoni mwa wiki wakati
akifunga Mashindano ya Umiseta kwa ngazi ya Mkoa yaliyofanyika katika Viwanja
vya Shule ya Sekondari Iyunga Jijini Mbeya, mashindano yaliyohusisha wachezaji
kutoka Kombaini ya timu za Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya.
Kaponda alisema mashindano hayo ambayo hufanyika
kuanzia ngazi ya Shule, Kata, Wilaya, Mkoa, Kanda hadi Taifa huwanyima fursa ya
kusoma wale ambao watabahatika kufuzu ngazi zote hizo hadi mashindano ya Taifa.
Kutokana na hali hiyo zaidi ya Wachezaji 40 wa
michuano hiyo waliochaguliwa kuunda timu ya Mkoa ni wanafunzi wa Kidato cha Nne
ambapo walitakiwa kukaa kambini kwa ajili ya kujiaandaa na mashindano katika
ngazi ya Kanda yatakayofanyika Hivi karibuni Mkoani Mbeya.
Aidha katika kilele hicho timu ya Kombaini ya
Jiji la Mbeya ilifanikiwa kuchukua Kombe la Mpira wa Miguu baada ya
kufanikiwa kutinga Fainali kwa kucheza na Timu ya Kombaini ya Wilaya ya Mbozi
na kushinda kwa jumla ya magoli 3 kwa moja.
Katika michuano hiyo timu hizo zilicheza kwa
kukamiana ambapo katika dakika ya 14 ya Mchezo huo Jiji ilifanikiwa kupata goli
la kuongoza lililofungwa na Christopher Edson, ambapo timu ya Mbozi
ilisawazisha goli hilo dakika ya 22 kipindi hicho hicho na kufanya timu kwenda
mapumziko zikiwa sare ya kufungana 1-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo
Christopher Mwaipopo aliifungia timu ya Jiji goli la pili kwa Mkwaju wa Penati
kufuatia kufanyiwa madhambi na mabeki wa timu ya Mbozi na Mwamuzi kuamuru
Mkwaju upigwe uliozaa goli katika dakika ya 72.
Dakika ya 90 Mbeya Jiji ilifanikiwa
kupata goli la tatu na la ushindi kutoka kwa mchezaji wake Ipyana Muyavilwa kwa
mkwaju wa Penati pia kutokana na kuangushwa katika eneo la hatari wakati mabeki
wa timu ya Mbozi wakijaribu kuokoa.
Zaidi ya michezo sita ilishindaniwa na kutolewa
makombe kwa washindi, zawadi ambazo zilizotolewa kwa ufadhili wa kampuni ya
vinywaji ya Pepsi kwa michezo ya Mpira wa Miguu kwa Wanaume na Wanawake, Mpira
wa Pete, Basketi Wanaume na wanawake, Voleyball wanaume na wanawake, Handball
Wanaume na Wanawake pamoja na mpira wa meza na riadha.
Aidha Afisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Juma Kaponda
baada ya kumaliza kukabidhi makombe kwa washindi pia aliwaambia washindi kuwa
makombe waliopewa ni vyao moja kwa moja hayatashindaniwa tena bali Mwakani
yataandaliwa mengine.
Picha na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment