WANACHAMA zaidi ya 40,000 wa zao la kahawa Wilayani Mbozi ambao walikumbwa na mtikisiko wa kiuchumi 2008/2009 wameiomba serikali kutekeleza ahadi iliyoitoa ya kulipa fidia kwa wakulima ambao walikumbwa na mdororo huo wa kiuchumi .
Mwaka 2008/09 serikali ilitenga na kutoa zaidi ya shilingi Trioni 1.7 kwaajili ya fidia ya mdororo ama mtikisiko wa uchumii uliozikumba baadhi ya kampuni lakini vikundi zaidi ya 200 vyenye wanachama 40,000 vya wakulima wa zao la kahawa wilayani Mbozi mkoani Mbeya bado wanasubiri fidia hizo.
Imeelezwa kuwa wakulima hao ambao hasa wanategemea zaidi kilimo,mpaka sasa wanadai fidia ya zaidi ya shilingi Bilioni, 8.0 ambazo zinatakiwa kuingizwa kwenye mabenki ambayo waliyakopa kwa wakati huo.
Wakulima hao wamesema kutokana na mtikisiko wa uchumi mpaka sasa hali zao ni mbaya kiuchumi,kwani baadhi ya benki ambazo wamekopa mikopo kwa wakati ule zimetangaza kuja kupiga minada nyumba zao,na kufilisi biashara zao.
Mbali na kufilisiwa biashara zao pia, mpaka sasa wakulima hao wamekosa sifa ya kukopa tena kwenye taasisi za kifedha kutokana na madeni waliyokopa kwa wakati huo, huku wamiliki wa makampuni wakilazimika kuhama makazi kwa kuogopa kupigwa na baadhi ya wakulima ambao hawajui nini maana ya kutikisika kwa uchumi.
‘’Tayari tumeshakusanya kiasi ambacho vikundi wanachama wa Umoja wa wakulima wa zao la kahawa wilayani Mbozi-MVIKAMBO vipatavyo 204,na kupata takwimu ya madai ya fidia ni shilingi zaidi ya Bilioni 8,tayari tumepeleka madai hayo kwenye ofisi ya waziri mkuu,Mizengo Pinda,ambaye ametujibu kuwa kabla ya kikao cha bunge kilichomalizika juzi hakijakwisha atakuwa ameshatupa jibu la hatima ya madai yetu ya fidia.’’alisema Fressy Mgalla.
Ferdy Mgalla ni mwenyekitii wa Umoja wa Vikundi vya wakulima wa kahawa wilayani Mbozi, mbaye aliliambia gazeti la Mtanzania kuwa mpaka sasa wakulima hao wanasubiri fidia za fedha zilizotokana na kudorora kwa uchumi duniani kulikosababisha bei ya zao la kahawa kuporomoka na kusababisha kahawa kwa soko la dunia kuuzwa kwa hasara.
Aidha wakulima hao, pia wameonesha msimamo wa kutoendelea kuuza kahawa mbichi(redchery) kwa kampuni zinazonunua kahawa hiyo kwakuwa zilikuwa zinawanyonya,kwani kilo tano ya kahawa mbichi ni kilo moja ya kahawa kavu.
Ukilinganisha kilo moja ya kahawa mbichi inauzwa shilingi 200,kilo tano ni shilingi 1,000,lakini kilo moja kavu ya kahawa ni shilingi 4,500 hadi 6,000 hivyo mkulima alikuwa anaibiwa shilingi 4,000 na 5,000 anapouza kahawa mbichi ya kilo tano.
|
No comments:
Post a Comment