Add caption
SHIRIKA la Umeme (Tanesco)Mkoa wa Mbeya
limefanikiwa kuwaunganishia umeme wateja zaidi ya 20000 kwa kipindi cha miezi
12 ikiwa ni juhudi za kufikisha asilimia 35 ya watanzania kupata huduma hiyo.
Hayo yalibainishwa jana na Meneja wa
Tanesco Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Maganga, katika mkutano wa wanachama wa Chama
cha Wakandarasi wazawa(TLCO) na Watumishi wa Tanesco uliofanyika katika ukumbi
wa Coffee Garden jijini hapa.
Maganga alisema Serikali iliweka
mikakati ili kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2015 asilimia 35 ya Watanzania wawe
wanauwezo wa kupata huduma ya umeme bila vikwazo hali iliyosababisha Shirika
hilo kufanya kazi usiku na mchana ili kufikia malengo hayo.
Alisema mafanikio hayo ni kutokana na
Shirika la Umeme kufanya kazi kwa ukaribu na Wakandarasi wa Mkoa wa Mbeya ambao
wamewezesha kufanya vizuri tofauti na mikoa mingine licha ya kuwepo kwa
changamoto chache ambazo alidai kuwa zinarekebishika.
Awali katika Mkutano huo, Chama cha
Wakandarasi (TLCO) kupitia kwa Raisi wake, Kura Mayuma, waliwatupia lawama
watumishi wa shirika la Tanesco Mkoa wa Mbeya kwa kuwabagua wakandarasi, kutoa
lugha chafu dhidi yao na hata kuwaita vishoka pindi wanapoonekana katika ofisi
za Tanesco kupata huduma.
Mayuma alisema mbali na watumishi hao
kuwaita wakandarasi vishoka lakini pia kuna baadhi ya watumishi wamekuwa
wakijihusisha na kazi za ukandarasi na kumiliki makampuni binafsi na kujipatia
kazi huku wakiwaacha wenye fani wakisota bila kazi licha ya kulipia leseni na
ada za ukandarasi.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment