WAANGALIZI wa kanisa la TAG jimbo
la kusini magharibi wamekabidhiwa pikipiki 15 zenye thamani ya shilingi Milion
54 ili kuwawezesha kuwafikia waumini wao kirahisi ikiwa ni pamoja na
utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka 10 ya mavuno ya kanisa hilo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi
pikipiki hizo, Makamu Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Magnus Mhiche, katika hafla
iliyofanyika kwenye kanisa la TAG Sokomatola jijini Mbeya, alisema hizo
pikipiki ni nyenzo ya kumfanya mchungaji kufanya kazi yake kwa ufanisi.
Alisema katika maadhimisho ya miaka 75
tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo kumekuwa na mikakati kadhaa ya kuhakikisha
Kanisa linavuna na kuongeza idadi ya waumini katika kuelekea miaka 75 mingine
hivyo pikipiki hizo ni moja ya kuhakikisha mpango huo unatekelezeka.
Aidha Makamu Askofu alitoa wito kwa
Wachungaji hao waliokabidhiwa pikipiki kuzitumia kwa kazi iliyokusudiwa na sio
kuzitumia kibiashara kwa kuwapa madereva wa bodaboda bali watumie katika kazi za
kanisa pekee pamoja na utunzaji ili zitumike kwa muda mrefu.
Aliongeza kuwa pikipiki hizo ni mali ya
Kanisa ambapo Mchungaji akiacha kazi atalazimika kuikabidhi kwa mrithi wake au
kiongozi wa Kanisa na sio kuifungia nyumbani kwake kwa madai ni mali yake
kabisa.
Hata hivyo alisema kabla ya kukabidhiwa
rasmi kwa mchungaji mmoja mmoja ni lazima wajifunze kuendesha na kupewa leseni
kabla ya kukaguliwa na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani ili wajue
sheria zote kuepuka ajali zisizokuwa za lazima.
Baadhi ya wachungaji waliokabidhiwa
pikipiki hizo walitoa shukrani kwa kanisa kwa kutambua ugumu wa kazi waliokuwa
wakiupata katika kutembelea makanisa yao kutokana na kuwa mbali na ugumu wa
usafiri kwa baadhi ya maeneo.
Mchungaji Moses Kaminyoge Mwangalizi wa
Mlowo Wilayani Mbozi alisema pikipiki hiyo itamsadia kuyafikia makanisa yake
yote kwa wakati muafaka pamoja na kufuatilia maendeleo ya mavuno ya miaka 10 ya
Tanzania kwa Yesu kikamilifu.
Naye Mchungaji Paulo Mfwomi mwangalizi
wa Tunduma Wilaya ya Momba alisema pikipiki husaidia maeneo ambayo hayafikiki
kwa usafiri wa gari hivyo itarahisisha kufika kila eneo kuwatembelea waumini
wake.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment