Mume na mke baada ya kukabidhiwa mtoto wao wakitoka katika ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya
Jeshi la
Polisi Mkoani Mbeya limemtia nguvuni mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la
Esther Amos(23) mkazi wa Nzovwe Jijini Mbeya kwa tuhuma za kuiba mtoto
mchanga jinsi ya kiume mwenye umri
wa miezi miwili.
Kamanda wa
Polisi Mkoani Mbeya Ahmed Msangi amesema mtoto huyo Yosia Jerome aliibwa Mei 14
mwaka huu alipokuwa na mama yake aitwaye Orester Shaban(24) aliyekuwa akiuza
mbogamboga katika soko la Ikuti Kata ya Iyunga Jijini Mbeya majira ya saa tatu
asubuhi.
Mbinu aliyoitumia
Esther ni kumrubuni mama wa mtoto kwenda kununua samaki huku akimkabidhi
shilingi elfu kumi kuwa mbali ya njegere alizonunua kwa Orester pia angehitaji
kupata samaki hivyo kumwachia mtoto ndipo alipotokomea naye kusiko julikana.
Kamanda
ameongeza kuwa mama wa mtoto alitoa taarifa Polisi kituo cha Iyunga na Kati
ambapo juhudi za kumtafuta mwanamke huyo zilianza na kufanikiwa kumpata Kijiji
cha Mahenje Wilaya ya Mbozi nyumbani kwa Dada yake Esther.
Baada ya
wasamaria wema kusikia taarifa za kuibiwa kwa mtoto wakazi wa Nzovwe walianza
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walianza kufuatilia taarifa za Esther
aliyedaiwa kujifungua na yupo kwenye mapumziko ya uzazi kwa Dada yake wilayani
Mbozi.
Askari
walifuatilia mwenendo wa Esther na kufanikiwa kumkamata Mei 18 mwaka huu majira
ya saa saba akiwa na mtoto na alipotakiwa kutoa maelezo alionekana kujikanyaga
na hata alipotakiwa kumnyonyesha alishindwa kufanya hivyo badala yake alitoa
chupa ya maziwa kwa ajili ya kumnyonyesha.
Baada ya
Askari kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa waliitwa wazazi wa mtoto kwa ajili ya
utambuzi wa mtoto na baada ya kumtambua Orester alizirai kutokana na kutoamini
kile kilichotokea machoni pake kupatikana mwanae akiwa hai.
Mtuhumiwa
alisafirishwa hadi Jijini Mbeya kwa mahojiano zaidi na Esther ambapo uchunguzi
umebaini kuwa katika maisha yake kabla ya kuolewa amejaliwa kupata mtoto wa
kike mwenye umri wa miaka tisa na alipoolewa hakujaliwa kupata mtoto ndipo
alipodanganya mume wake kuwa ana ujauzito ambapo amekwenda kwa Dada yake
kujitazamia.
Mtoto Yosia
alifikishwa Hospitali ya Wazazi ya Meta na kwamba Afya yake inaendelea vema.
Kamanda wa
Polisi alimkabidhi mtoto kwa wazazi wake Ofisini kwake mbele ya Waandishi wa
Habari na Maafisa wa Polisi ambapo alitoa wito kwa wazazi kuwa makini na watoto
wao na kutowakabidhi watu wasiowafahamu pia waendelee kushirikiana na Polisi
ili kukomesha uhalifu Mkoani Mbeya na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Kwa upande
wake Baba wa Mtoto Jerome Nzowa amelishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano
mkubwa hata kufanikisha kupatikana kwa mwanae akiwa hai na salama.
Na Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment