SHULE mbalimbali za msingi katika mji wa
Tunduma wilaya ya Momba Mkoani Mbeya zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa
watoto madarasani kutokana na ukosefu wa madawati na madarasa.
Hayo yamebainika katika ziara ya Katibu
wa CCM kata ya Tunduma, Hemed Stephen alipotembelea baadhi ya shule katika kata
hiyo Januari 15,mwaka huu akiambatana na kamati ya siasa na uchumi.
Katika ziara hiyo ambayo aliongozana na
Afisa Elimu wa mji wa Tunduma Franco Ngonya ilimpelekea kutembelea shule
za Manga Mwaka na Mkombozi ambapo alishuhudia changamoto hizo.
Alisema katika shule ya msingi Mwaka
yenye jumla ya wanafunzi 1727 ikiwa na walimu 22 tu huku ikiwa na vyumba 11 vya
madarasa ambapo ina upungufu wa vyumba 19 hali inayolazimu walimu kufundisha
kwa awamu mbili asubuhi na mchana ili kila mtoto aweze kusoma.
Alisema walimu wanakabiliwa na
ukosefu wa ofisi ya walimu na samani ambapo mwalimu mkuu wa shule ya Manga
iliyopo Mwaka Betina Timoth alimweleza Katibu kuwa shule yake inakabiliwa na
upungufu wa madawati 268 na walimu 59 hivyo hulazimika kufundisha watoto zaidi
ya mia katika kila darasa badala ya 45 kama ulivyo utaratibu.
Kutokana na upungufu wa vifaa vya ofisi
ya Walimu Katibu huyo alitoa viti vitano kwa ajili ya ofisi ya walimu.
Katibu aliendelea na ziara yake katika
shule ya Mkombozi ambapo alishuhudia darasa moja likiwa na watoto 350 huku
baadhi ya watoto wakiwa wameeti chini kwa ukosefu wa madawati na vyumba vya
madarasa na kujionea madarasa yaliyokwama kuezekwa kutokana na ukosefu wa fedha
baada ya wazazi kujenga hadi mtambaa panya.
Pia alisomewa risala na mwalimu mkuu
Simika Hakton ambaye alimwambia katibu na ujumbe wake kuwa wanakabiliwa
na changamoto ya samani za walimu hali inayowafanya walimu kufanya kazi katika
mazingira magumu.
Hata hivyo Katbu alimtaka Afisa Elimu
kutoa kipaumbele kwa shule hiyo kuezekwa kwa madarasa ambapo alikiri kutengwa
shilingi milioni 45 zitakazogawanywa shilingi Milioni 10 kila moja kwa shule za
Mwaka,Mkombozi,Uhuru na Migombani ili kupunguza msongamano madarasani.
Alihitimisha ziara yake shuleni hapo kwa
kutoa mchango wa shilingi 232,000/- kwa ajili ya kupunguza kero ya samani
shuleni hapo ambapo mwalimu Simika alimshukuru Katibu kwa moyo wa uzalendo na
kuahidi kuzitumia kwa malengo yalikusudiwa.
Mwisho.
Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu
|
1 comment:
IDADI HIYO YA WANAFUNZI NDANI YA DARASA MOJA HAIKUBALIKI NA NDIYO CHANZO CHA ELIMU KUPOROMOKA.
Post a Comment