MKUU wa Mkoa wa Mbeya Bw. Abbas Kandoro, amesema mafisadi wanaoiba dawa za Serikali, kuzipeleka kwenye maduka ya watu binafsi na kusababisha uhaba mkubwa wa dawa katika Bohari Kuu (MSD), hawawezi kuvumiliwa. Bw. Kandoro aliyasema hayo mjini Mbeya wakati akifungua warsha ya siku moja iliyoshirikisha wadau wa MSD kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Iringa na Njombe.
Alisema Serikali imekuwa ikishuhudia uhaba mkubwa wa dawa uliopo MSD wakati maduka binafsi yanauza dawa za Serikali ambazo haziruhusiwi kuuzwa katika maduka hayo.
“Kimsingi Serikali inatumia mabilioni ya fedha kuhakikisha MSD inakuwa na dawa za kutosha ambazo zitasambazwa katika hospitali ili ziweze kuwasaidia Watanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapaswa kufanya uchunguzi katika maduka binafsi kubaini mafisadi wa dawa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.
Bw. Kandoro alisema tabia ya wizi wa dawa unafanywa na watu wasio na nia njema na uchumi wa nchi ambao unategemea watu wenye nguvu na afya bora hivyo kinachotakiwa kufanya uchunguzi ili kuwabaini watu wanaofanya ufisadi wa kuiba dawa MSD.
“Nawaonya wauzaji dawa katika maduka binafsi kuacha tabia ya kuuza dawa zilizopita muda wake, kitendo hiki ni sawa na uuaji kwani matumizi yake ni sawa na sumu mwilini hivyo kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji kiafya,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kanda, Bw. Cosmas Mwaifwani, alisema MSD imejipanga kuhakikisha inawahudumia Watanzania kwa kiwango stahiki na kukidhi mahitaji yao.
Alisema katika mpango wa muda mfupi, wamejipanga kuhakikisha wanakuwa na utaratibu wa kufikisha dawa hadi vituo vya afya kwa ajili ya kumaliza tatizo la upungufu na upatikanaji wa dawa.
Aliongeza kuwa, mawakala wamekuwa wakichelewa kupeleka maombi ya dawa MSD hivyo kusababisha zisipatikane kwa wakati.
Na Charles Mwakipesile, Mbeya picha na joseph mwaisango |
No comments:
Post a Comment