Wanatajati wakiwa juu ya Telezo ambalo liko tayari kwa ajili ya kuanza kujengea Meli kubwa ya abiria ujenzi unaotarajiwa kukamilika Mwezi Februari mwakani. |
Moja ya Meli ya Mizigo inayotarajia kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu ikiwa katika hatua za ufungaji wa mitambo |
Muonekano wa Chelezo |
Wanatajati wakishuka kwenye Telezo |
Mafundi wakiendelea na kazi |
WanaTAJATI wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilisha ziara. |
MRADI wa Ujenzi wa Meli tatu
katika Bandari ya Itungi iliyopo Kyela Mkoa wa Mbeya unaofanywa na Mkandarasi
mzawa kutoka kampuni ya Songolo Marine Transport Botyard umegeuka kuwa Chuo cha
ufundi kwa vibarua wanaosaidia kazi.
Akizungumza na Waandishi wa
habari kutoka Chama cha Waandishi wa habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania (TAJATI)
waliofanya ziara katika Bandari ya Itungi juzi, Mkurugenzi na mmilikiwa Kampuni
ya Songolo Marine, Salehe Songolo alisema ndoto yake ni kuona anaeneza taaluma
ya ufundi kwa vijana wengi.
Alisema kawaida vijana
huajiriwa kama vibarua kwa ujira wa kuanzia shilingi Laki mbili lakini wakati
huo huo huendelea kujifunza kazi za ufundi kasha hupandishwa daraja kulingana
na uelewa wake na kwamba mtu ambaye hawezi kujifunza humfukuza kwa kuwa anakuwa
amekosa malengo.
Alisema katika Miradi mitatu
aliyokabidhiwa na Serikali Mwaka jana Oktoba ambayo inatarajia kukamilika
Februari mwakani, vijana zaidi ya 100 wakazi wa Kyela wanatarajia kunufaika na
elimu ya ufundi wanayopata kutoka kwa Mkandarasi huyo hadi kukamilika kwa
miradi.
Aliitaja miradi inayotekelezwa
bandarini hapo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Chelezo uliokamilika kwa asilimia 95 uliyogharimu
shilingi Bilioni 2.99 kuanzia usafirishaji kutoka Mwanza hadi Kyela na uundaji
wake.
Alisema Mradi mwingine ni
utengenezaji wa Meli mbili za Mizigo zenye uzito wa tani 1000 na uwezo wa
kubeba mizigo tani 566.166 kila moja ambazo zitagharimu shilingi Bilioni 11.253
na kwamba moja ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 75 na inatarajiwa kuanza
kutumika mwezi Agosti Mwaka huu na nyingine iliyofika hatua ya asilimia 50
itakayokamilika mwezi Oktoba mwaka huu.
Songolo alisema mradi wa tatu
ni ujenzi wa Meli ya Abiria na mizigo ambayo hadi sasa imefikia asilimia 30
inayotarajia kukamilika mwezi Februari mwakani inayogharimu shilingi Bilioni
10.35, na kuongeza kuwa ikikamilika itakuwa inauwezo wa kubeba abiria 200
pamoja na magari madogo 12 au makubwa na madogo matatu matatu kwa wakati mmoja.
Mkandarasi huyo alisema
changamoto kubwa aliyokutana nayo ilikuwa ni mfumo ambao alitakiwa kujenga
melihizo kuwa mpya na mgumu tofauti na mifumo aliyoitumia katika meli 48
alizozijenga nchini ambazo husimamiwa na Sumatra hivyo kuwa rahisi kuimuda kazi
hiyo.
Alisema Meli zinazojengwa Kyela
zinamfumo wa Nje na kusimamiwa na Wabelgiji hivyo alitakiwa kwenda kuchukua
vibarua nchini India ambako ndiko walikozoea mfumo huo lakini kwa sababu ya
uzalendo aliona ni vema kuwachukua vibarua wazawa kuwafundisha mfumo huo mpya
kabla ya kuanza mradi ili taaluma ibaki nchini.
Alisema katika ujenzi huo jumla
ya wafanyakazi 104 ambao 38 wanatoka Mkoani Mwanza na wengine wote wakitokea
Kyela huku akiwa na Raia wa Kigeni wawili ambao mmoja wao ni mwalimu wa
kufundisha vijana na mwingine akisaidia mawasiliano kati ya Kyela na Ubelgiji
ambao ndiyo wasimamizi.
Baadhi ya vibarua walisema
wanajivunia kupata kazi katika ujenzi wa Meli hizo kwani baada ya kukamilika
kwa mradi wanauhakika wa kufungua ofisi zao katika fani mbali mbali ikiwemo
uchomeleaji na uunganishaji wa vyuma pamoja na kukata.
No comments:
Post a Comment