Mkurugenzi wa Mradi wa PS3 Dk. Emmanuel Malangalila akitoa taarifa ya Mradi huo katika hafla ya uzinduzi wa Mradi iliyofanyika katika ukumbi wa Royal Tughimbe jijini Mbeya. |
Mratibu wa Mradi wa PS3 Beatha Swai akieleza malengo na matarajio ya mradi huokwa Halmashauri za Mkoa wa Mbeya |
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma uliozinduliwa kimkoa jijini Mbeya |
Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) Shanon Young akitoa neno katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa PS3 ambao umedhaminiwa na Serikali ya Marekani |
Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja (aliyesimama) akitoa utambulisho wa wageni katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa PS3 |
Wakuu wa Idara na viongozi mbali mbali wakifuatilia shughuli za uzinduzi wa Mradi katika ukumbiwa Tughimbe Mafiati jijini Mbeya |
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Munasa akitoa neno la shukrani baada ya hotuba ya mgeni rasmi |
Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja |
Viongozi wakiagana |
Washiriki wakiwa kwenye ukumbi wa Mikutano |
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos
Makalla amesema uimarishwaji wa mifumo ya sekta za Umma nchini utasaidia
kuondoa tatizo sugu la watumishi hewa endapo utekelezaji wake utafanyika
vizuri.
Makalla aliyasema hayo
alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mradi wa Uimarishaji mifumo ya Sekta
za Umma mkoani Mbeya uliofadhiliwa na shirika la Msaada la Marekani (USAID)
katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Royal Tughimbe jijini Mbeya.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema Mradi
huo umekuja katika kipindi muafaka ambacho serikali ya awamu ya tano
inajitahidi kuhakikisha inahimiza na kurekebisha iliyokuwepo katika Sekta za
Umma ili kurahisisha utoaji huduma bora kwa wananchi.
Alisema Mradi huo utasaidia
kuweka mfumo mzuri ambao utaondoa kabisa tatizo la watumishi hewa katika
taasisi za umma na kuboresha mfumo wa utendaji kwa watumishi kutimiza wajibu
wao kwa kiwango chenye ubora na wakati unaostahili.
Awali akisoma taarifa katika
uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mradi, Dk. Emmanuel Malangalila alisema mradi huo
utahakikisha mifumo iliyopo katika ngazi ya Halmashauri inaimarishwa kupitia
kitita cha afua zilizoundwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa
wananchi wa Tanzania.
Dk. Malangalila alisema mradi
huo unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2015 hadi 2020 ambapo
mafanikio yanategemewa kutokea kwenye sekta ya Utawala bora na ushirikishwaji
wa raia ambapo Rasilimali za taifa zitatumika kwa uwazi, kuwawezesha ushiriki
wa wananchi katika kupanga, kufuatilia na kutoa matokeo katika kila sekta.
Alisema mafanikio mengine ni
kuongezeka kwa usawa katika mgawanyo wa rasilimali watu kwa ajili ya utoaji wa
huduma bora kwenye maeneo yenye uhitaji zaidi, kuimarisha mfumo wa ajira pamoja
na kudumu kwa watumishi katika ajira serikalini.
Aliongeza kuwa mradi huo pia
utasaidia ongezeko la pato la ndani kwa ajili ya huduma za umma, kuongezeka kwa
ufanisi katika matumizi ya fedha za umma pamoja na kuongeza uwiano kati ya
kiasi cha fedha kilichotumika na mali iliyonunuliwa jambo ambalo litapunguza
hati chafu na zenye mashaka kwenye halmashauri.
Dk. Malangalila alisema
kuimarishwa kwa mifumo ya utoaji taarifa iliyopo nchini pamoja na matumizi ya
takwimu kwa wadau utasaidia kutokuwa na takwimu za kutengenezwa ambapo pia
Mradi huo utasaidia katika tafiti tendaji zitakazosaidia mradi kujua changamoto
na mikakati ya kuzishughulikia
changamoto hizo.
Kwa upande wake Mratibu wa
Mradi huo kutoka Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi, Beatha Swai alisema Mradi
huo unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania Bara ambayo ni Iringa, Dodoma,
Kagera, Kigoma,Lindi, Mara,Mbeya, Morogoro, Mtwara,Mwanza, Njombe, Rukwa na
Shinyanga.
Alisema uzinduzi wa mradi huo
umeshafanyika katika Mikoa ya Iringa, Shinyanga, Dodoma na Morogoro huku Mikoa
ya Mtwara, Mwanza na Mbeya ikizindua kwa pamoja ambapo alisema mategemeo ya
Wizara ni kuwa mradi huo utasaidia kuwajengea uwezo watumishi wa Halmashauri
katika utekelezaji wa majukumu yao.
No comments:
Post a Comment