Kapten Sambwee Shitambala akiwa katika moja ya mikutano ya Kampeni wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. |
Kwanza napenda kutoa
shukurani kwa Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia sote kumaliza kampeni na uchaguzi
kwa usalama na amani bila kuibuka kwa vurugu za aina yoyote. Na hiii ilikuwa
kauli mbiu yangu amani na usalama ndo msingi wa maendeleo ya nchi na jimbo letu.
Pili natoa shukurani kwa
chama cha MapinduzI kwa kuniteua kupeperusha bendera ya chama changu katika
uchaguzi mkuu kugombea ubunge jimbo la Mbeya mjini ambao ulihitimishwa Oktoba
25.
Pia nawashukuru
wanahabari kwa msaada wao katika kuujuza umma wa Mbeya mambo yaliyokuwa
yakijiri kwenye kampeni zetu tulizokuwa tukizifanya kwenye kata zote 36,
nilifanikiwa kufanya jumla ya mikutano 56 na zaidi ndani na nje na niliweza
kukutana na wananchi wengi maeneo mbalimbali niliyofanya kampeni na kusikiliza
kero zao.
Nachukua fursa hii pia
kuwashukuru wagombea wenzangu wote wa ndani ya chama wapatao 15 kwa
kushirikiana nami katika Kampeni hizo. Shukrani za pekee zimwendee Charles
Mwakipesile aliyekuwa Meneja wangu.
Pamoja na mimi kuteuliwa
na chama bado wagombea wenzangu katika chama walijitahidi kuniunga mkono na
kunisapoti kwa hali na mali wapo walioacha shughuli zao na kuzunguka nami
kwenye kampeni zote jitihada zao zimeonekana, nawashukuru sana.
Navishukuru kipekee
vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa, ngumu na nzuri waliyoifanya na
kulifanya jiji letu la Mbeya kuwa salama hadi leo. Nawashukuru sana.
Nilijitahidi kufanya
kampeni za kistaarabu, kwa kutumia uwezo wangu wote pamoja na matukio
mbalimbali ya kejeli yaliyokuwa yakitolewa na wapinzani wetu, nilichukulia kama
ndio siasa kwani kila mmoja alikuwa anatafuta kiti cha Ubunge wa Jiji la Mbeya
kwa namna yake lengo letu lilikuwa moja kusukuma maendeleo ya Jiji letu.
Mwenzangu wa chadema
ameibuka na kura nyingi zaidi ya wengine tuliogombea naye na kutangazwa kuwa
mbunge mteule wa jiji la Mbeya. Haya ni maamuzi ya wana Mbeya wengi zaidi ya
wale waliotaka niwe mbunge wao. Nampongeza Sugu kwa ushindi huo na pia
ninamtakia kila laheri katika muda wake wa uongozI. Pamoja na dosari
zilizojitokeza kwenye uchaguzi huu lakini nimekubaliana na matokeo, tuweke
mambo ya itikadi pembeni tusimame pamoja tuijenge Mbeya yetu.
Kwa bahati mbaya sana
nimeshindwa katika uchaguzi huu nikiwa nimekusanya takribani kura 50,000
inawezekana wakati bado haujafika wa mimi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya,
nimefarijika kwa wale walionipa kura na hata wale ambao hawakunichagua,
Nawashukuru wananchi wote.
Najua walionichagua
walinielewa, walinikubali,walihitaji niwawakilishe. Nasema nitawawakilisha na
sitowatupa. Yale niliyoyasema yatatimia juu yao kwa namna moja ama nyingine
kadri Mungu atakavyojalia. Sitawaacha wala kuwaangusha. Nawaomba wasijione
wameshindwa na wasikate tamaa. Nipo nao pamoja. Ahadi nilizotoa wakati wa
kampeni nitazitekeleza kwa kadri ambavyo Mungu atanijaalia.
Nipo na wanajamii hapa
hapa Mbeya, shughuli zangu na biashara zangu zipo hapa Mbeya nitaendelea kuwa
na wana Mbeya kwa hali na mali tukiendelea kulijenga Jiji letu la Mbeya.
Naahidi nitaendelea
kushirikiana na wananchi wa jimbo la Mbeya kwa hali na mali nikifuatilia na
kutekeleza ahadi zilizoahidiwa na Rais mteule Dkt.John Pombe Magufuli, pamoja
na kwamba sikuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Mbeya.Kwa niaba ya walionipigia
kura nitafanya kazi.
Ndugu wanahabari nilijiwekea
vipaumbele wakati wa kampeni zangu pamoja na ahadi kwa wananchi wa jimbo la
Mbeya katika baadhi ya maeneo niliahidi mambo mbalimbali kama vile ujenzi wa
zahanati kata ya Iyunga, Igawilo, Ilemi na Nsoho. Shule kata ya Iziwa, na
zinginezo, usafiri wa daladala pembezoni, maji na umeme. Pia kutafuta waalimu
wazuri kwa ajili ya shule zetu. Bila kusahau pembejeo kwa wakati.
Nitashirikiana na wananchi katika kutekeleza ahadi zangu.
Pia zipo ahadi
nilizoahidiwa na Rais wangu mteule ambaye ni muadilifu na mchapakazi
nitamkumbusha ikiwemo km 10 za barabara Jiji la Mbeya na mengineyo ambayo
nimeahidi kuyatekeleza mwenyewe kwa wapiga kura wakati wa kampeni.
Ndugu zangu wanahabari,
naamini mlikuwa mkitafakari kukaa kwangu kimya baada ya kumalizika kwa uchaguzi
huu wengi walitegemea ningeweza kupinga matokeo, kufanya hivyo kungesababisha
kuchelewesha mahitaji ya wakazi wa jiji la Mbeya ambao wanahitaji huduma yangu
na ahadi nilizotoa kwa wengi waliojitokeza kuniunga mkono, nawaahidi
sitawaangusha.
Mwisho lakini si kwa
umuhimu napenda kuwasisitiza wakazi wa Jiji la Mbeya kuendelea kushikamana kwa
ajili ya kuliendeleza jiji letu, tuepuke vishawishi na kujiingiza katika mambo
ya uvunjifu wa amani na utulivu.
Amani ya Mbeya ikitoweka
hakuna biashara inayoweza kufanywa wala hakuna shughuli zozote za maendeleo
ambazo zinaweza kufanywa,vijana wajikite kwenye ujasiriamali watafute riziki
yao halali kwa kuwa Mbeya yenye amani na salama kwa Maendeleo yetu linawezekana.
Ahsanteni
Capt. Sambwee Shitambala (MNEC-CCM, Mbeya)
No comments:
Post a Comment