Uhamiaji Mbeya
IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Mbeya
inawashikilia wahamiaji Haramu 62 ambao ni Wahabeshi raia wa Ehtiopia pamoja na
Watanzania wawili wakituhumiwa kuingia nchini kinyume na utaratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisinin kwake Afisa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya, William Bambanganya alisema
watuhumiwa hao wote wameshafunguliwa mashtaka ya kuingia nchini bila kufuata
sheria huku Watanzania wawili wakishtakiwa kwa kuhusika kuwasafirisha Wahamiaji
haramu.
Alisema wahamiaji hao walikamatwa katika
matukio mawili kutokana na kupata taarifa kutoka kwa Watanzania ambao hawapendi
vitendo vya kujihusisha na usafirishaji wa Wahamiaji haramu kinyume na taratibu
hivyo kukiwezesha kikosi cha Uhamiaji kuwatia mbaroni kirahisi.
Alisema katika tukio la kwanza
lililotokea Februari 8, mwaka huu ambapo Jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka
kwa raia wema zikisema kuna wahamiaji haramu katika moja ya Nyumba za wakazi wa
kitongoji cha Mwaka katika Mji mdogo wa Tunduma Wilaya ya Momba mkoani Mbeya.
Alisema baada ya kufika eneo la tukio
walifanikiwa kuwakamata Wahabeshi 45 raia wa Ethiopia pamoja na Mtanzania mmoja
aliyefahamika kwa jina la Shukrani Sastoni wakiwa katika nyumba ya Elisha
Mwazembe usiku majira ya saa sita.
Aliongeza kuwa Mwenye nyumba hawakufanikiwa
kumkamata ingawa Washtakiwa wote walifikishwa Mahakamani na utaratibu wa
kumtafuta mwenye nyumba bado unaendelea huku hatua za kisheria za
kutaifisha nyumba hiyo kuwa mali ya Serikali zikiwa zinafanyika.
Alisema tukio la pili lilitokea Februari
11, Mwaka huu majira ya saa 11 asubuhi katika eneo la Mbozi ambapo Wahamiaji 17
raia wa nchini Ethiopia walikamatwa wakiwa kwenye gari aina ya Noah lenye
namba za usajili T 340 BUP likiendeshwa na Lugano Albert.
Alisema mbinu iliyotumika ni Dereva wa
gari hilo kutaka kusimama kwa kificho katika moja ya nyumba iliyojitenga peke
yake akidhani pana usalama bila kujua nyumba hiyo inakaliwa na watu na kujikuta
wakiwekwa chini ya ulinzi na maafisa Usalama wa Taifa ambao ndiyo waliokuwemo
kwenye hiyo nyumba.
Aliongeza kuwa tayari watuhumiwa hao
wamefikishwa katika vyombo vya sheria wakisomewa mashtaka ya kuingia nchini
bila kibali huku Mtanzania ambaye alikuwa ni dereva akisomewa mashtaka ya
kuwasafirisha wahamiaji haramu kinyume cha Sheria huku taratibu za kulitaifisha
gari hilo kuwa mali ya Serikali zikiendelea.
Afisa huyo aliongeza kuwa utaratibu wa
kutaifisha mali au kitu kinachohusika na Wahamiaji haramu utasaidia kupunguza
wimbi la uhamiaji haramu hapa nchini ingawa alikiri kuwepo kwa ongezeko la
wahamiaji kwa kipindi cha Mwezi huu ukilinganisha na Mwaka jana.
Alisema Februari 2, Mwaka huu
walikamatwa wahamiaji 15 raia wa Burundi ambao walifanikiwa kuwarudisha nchini
kwao, na kuongeza kuwa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mbeya iko katika Mazungumzo na
Uhamiaji Mikoa mingine ili kuangalia mianya wanayopitia kabla ya kufika Mkoa wa
Mbeya ambapo wanavuka mikoa mingi kabla ya kufika.
Picha na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment