MAMLAKA
ya udhibiti wa chakula,dawa na vipodozi(TFDA) kanda ya nyanda za juu kusini
imezifunga machinjio mbili Mkoani Mbeya kutokana na kuwa na kasoro za kiafya.
Machinjio
hizo ni Uyole iliyopo Jijini Mbeya na Mbalizi iliyopo katika Wilaya ya Mbeya
Mkoani hapa kutoka na kukithiri kwa uchafu.
Kaimu
Meneja wa Kanda nyanda za juu Kusini,Rodney Alananga, alithibitisha kufungiwa
kwa machinjio hizo na kwamba sababu za kufunga machinjio ya Uyole Jijini Mbeya
ni kutokana na kutokuwa na miundo mbinu mizuri ya maji hivyo kuhatarisha
afya za walaji na wakazi walio kando ya machinjio.
Alananga
amebainisha kuwa machinjio hiyo haina uzio na kufanya watu wasiohusika kuingia
machinjioni kinyume na sheria kwani watu wanaopaswa kuingia ndani ya machinjio
ni wahusika tu.
Alisema
kabla ya kufunga machinjio hayo ya Uyole mara kadhaa waliongea na uongozi
wa Jiji la Mbeya lakini hawakutekeleza maagizo waliyopewa mara kwa mara na
hivyo Mamlaka kuamua kuifunga ili kuokoa afya za wananchi wasikumbwe na
magonjwa kama kuhara na kipindupindu.
Alisema
sababu nyingine ni kujaa kwa mashimo ya maji machafu kutokana na kutokunyonywa
kwa muda mrefu hali inayosababisha harufu mbaya eneo hilo na maeneo
yanayozunguka na kuleta uchafuzi wa mazingira Jijini.
Kwa
upande wa Machinjio ya Mbalizi, Alananga alisema sababu za kufunga ni
pamoja na wafanyakazi wa Halmashauri kutokuwa na sare za kufanyia kazi kama
viatu vyeupe,kofia na makoti meupe kama sheria inavyoagiza.
Alisema
kuwa hali ni mbaya zaidi katika machinjio hiyo kutokana na mashimo kujaa kwa
muda mrefu hivyo maji machafu na taka kufurika na kutiririsha uchafu mto
Mbalizi na kuwafanya wananchi wanaotumia maji ya mto huo kuwa hatarini kukumbwa
na magonjwa kutokana na wengine huyatumia kunywa kutokana na uhaba wa maji
ya bomba bonde la Mbalizi.
Kutokana
na hali hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Magreth
Akilimali, alilazimika kutembelea na kujionea hali halisi ya uchafu uliokithiri
na kuahidi kuwa watafanya usafi eneo hilo kwa muda wa siku tano kuanzia Desemba
14 kwa kutumia gari la kunyonya maji machafu la Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Hata
hivyo Akilimali, alipoulizwa sababu za kufungwa Machinjio hakuwa
tayari kuongea eneo la tukio na kudai kuwa afuatwe ofisini kwake ambapo aliamua
kuingia katika gari lake na kuondoka eneo la tukio.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa machinjio ya Mbalizi, Simon Petro(Mwadada) alisema
amesikitishwa na kitendo cha kufungwa kwani kitendo hicho kimewatia hasara
kubwa kwa madai kuwa itawalazimu kutumia zaidi ya shilingi elfu sitini kwenda
kuchinja machinjio ya Mjini au Songwe.
Baadhi
ya wafanya biashara ya nyama eneo la Mbalizi akiwemo Sikujua Mwambambe
ameishukia Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kutofanya usafi licha ya
Madaktari wa mifugo kupima nyama kila siku na kukusanya ushuru hali inayoonesha
kuna hali ya uzembe na uwajibikaji hafifu kutokana na taarifa zimepelekwa
ofisini lakini hakuna utekelezaji wowote.
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Mbeya, Anderson Kabenga, amekiri kufungwa kwa machinjio hiyo
na kwamba amemwagiza Mkurugenzi kufanya zoezi la usafi haraka ili kuondoa
usumbufu kwa wakazi wa Mbalizi na kitendo hicho kinaipunguzia mapato
Halmashauri.
Kabenga
alisema wanatafuta machinjio mbadala ili huduma za uchinjaji ziendelee katika
kipindi hiki cha ukarabati.
Kwa
upande wake Kaimu Meneja wa TFDA kanda ya nyanda za juu Kusini, Alananga
alisema zoezi hilo ni kutekeleza sheria ya chakula,Dawa na vipodozi
sheria namba 41,43 na 44 ya mwaka 2003 na kwamba Mamlaka itaendelea kufanya
ukaguzi katika maeneo mengine.
Mamlaka
hiyo kwa siku za hivi karibuni imeteketeza vyakula,dawa na vipodozi hatari
vilivyokwisha muda wake na vilivyoingizwa nchini kinyume cha sheria katika
wilaya za Momba,Kyela na Jijini Mbeya.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment