rubani wa ndege Andreas Daffee. akipongezana na wakili wake Lweikaza |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mbeya,
imewaachia huru watuhumiwa watatu ambao ni Mwekezaji wa Shamba la
Kapunga(Kapunga Rice Project) lililopo Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya ambao
walikuwa wakituhumiwa kwa mashtaka matatu ambayo ni kula njama,
kumwaga sumu na kuharibu mashamba ekari 557 ya Wananchi.
Akisoma hukumu Mhakamani hapo, Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite alisema upande wa mashtaka umeshindwa
kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili watuhumiwa ambao ni Waldeman
Veemark ambaye ni meneja wa shamba, Sergei Beacker ambaye ni Afisa Ugani wa
kampuni pamoja na rubani wa ndege Andreas Daffee.
Mteite alidai kuwa mbali na upande wa
mashtaka kuwa na mashahidi 155,ambapo kati yao mashahidi zaidi ya 20 hawakuweza
kufika mahakamani huku wengine 9 wakitoa ushahidi wa uongo tofauti na mashtaka
yaliyopelekwa.
Aliongeza kuwa katika mashahidi hao,
Shahidi wa 102 ambaye ni Mtaalam wa Kilimo wa kijiji cha Kapunga
aliyefahamika kwa jina moja la Geophrey alishindwa kuithibitishia Mahakama
utaalamu wa kimaabara kwamba kilichomwagwa na watuhumiwa hao ni sumu.
Hakimu huyo alisema pia mashahidi hao
zaidi ya 100 hakuna aliyekiri kuwaona washtakiwa wakitenda kosa hilo licha ya
kudai waliiona ndege ikiwa angani ikinyunyiza vitu vinavyodhaniwa kuwa ni
sumu.
Kutokana na ushahidi huo Hakimu Mteite
alisema Mahakama inawaachia huru washtakiwa wote watatu kwa mujibu wa kifungu
cha 312 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Awali mwendesha mashtaka wa Serikali,
Archiles Mulisa alidai mahakamani hapo kuwa Watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda
kosa hilo Januari 12, 2012 kinyume cha sheria namba 336 na kifungu cha 122(i),
sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Ambapo walidaiwa kuharibu ekari 557.5 za
mashamba ya mpunga ya wananchi yenye thamani ya shilingi zaidi ya Milion 800
kwa kumwaga dawa inayodaiwa kuwa ni sumu kwenye maji na mazao hali
iliyowaathiri kiafya baadhi ya wananchi.
Kwa upande wa washtakiwa ambao walikuwa
wakitetewa na Wakili Ladislaus Lwekaza, ambapo wakiwawanajitetea walisema
kwamba hawakuhusika na tukio hilo na kwamba siku ya tukio Meneja alikuwa
ofisini ili hali washtakiwa wengine walidai kuwa hawakuwepo eneo la tukio.
Hata hivyo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Mbeya, Michael Mteite alimaliza kusoma hukumu hiyo kwa kutoa
nafasi kwa upande wa mashtaka kukata rufaa kwa mujibu wa sheria kutokana na
kuwa wazi kama hawakuridhika na hukumu.
Picha na Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment