MSHIKEMSHIKE wa Jina la Mkoa Mpya utakaogawanywa
kutoka Mkoa wa Mbeya umezidi kushika kasi baada ya kila pande kupendekeza
majina kutokana na maeneo wanayotoka.
Sakata hilo limetokea hivi karibuni baada ya
Halmashauri ya Wilaya ya Momba wakitaka Mkoa huo kuitwa jina la Momba huku
Wilaya ya Mbozi ikipendekeza Mkoa Mpya uitwe Songwe.
Wakizungumza katika Baraza la Madiwani la
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi lililofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo
walisema sababu ya kuitwa kwa Songwe kunatokana na Mto Songwe kupitia Wilaya
zote ambazo zitaunda Mkoa Mpya.
Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Elisey Ngoyi
alitoa taarifa hiyo huku akitaja Wilaya zitakazounda Mkoa Mpya kuwa ni Mbozi,
Momba, Ileje, Chunya, Mbalizi na Igamba ambazo zote zinapitiwa na Mto Songwe.
Pia alipendekeza Makao makuu ya Mkoa huo kuwa
Tarafa ya Vwawa Wilayani Mbozi kwa kile alichodai kuwa ni katikati ya Wilaya
Zote hali itakayowarahisishia wananchi kutembea kwa muda mfupi kutoka Kila
Wilaya.
Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Baraza zima la
Madiwani chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ambakisye Minga walisema hali
ya miundombinu ni nzuri katika kila Wilaya zilizopendekezwa na kwamba Wilaya ya
Chunya igawanywe kufuata majimbo ya Uchaguzi kwa Jimbo la Lupa liwe Mkoa
wa Mbeya na Songwe kuwa mkoa wa Songwe.
Waliongeza kuwa katika Wilaya hizo
zinashabihiana katika mambo mengi yakiwemo Shughuli za kiuchumi , utamaduni ,
uoto wa asili, ukubwa Kijografia na mazao ya kilimo ambayo hulimwa na kustawi
katika Wilaya kama vile Kahawa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya
Mbozi, Charles Mkombachepa aliwashukuru madiwani kwa michango yao na kwamba
Mchakato huo utapelekwa katika Baraza la Ushauri la Wilaya kwa ajili ya
kujadiliwa na kupelekwa baraza la Mkoa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Dk. Michael Kadeghe
aliwataka wajumbe watakaohudhuria Baraza la Ushauri kusimamia maamuzi
yaliyopendekezwa na madiwani yasije yakabadilishwa na kuwakosesha raha wananchi
kwa mawazo yao kupitia wawakilishi wao ambao ni madiwani.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya Dk. Kadeghe
alitumia Fursa kupiga marufuku uuzaji na ununuaji wa kahawa mbichi maarufu kwa
jina la Cherry Wilayani humo kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara
kuanza kuwarubuni wakulima.
Alisema wakulima hao hurubuniwa kwa kuuza kahawa
hiyo kwa bei ya chini hali ambayo inadidimiza uchumi na kwamba hali hiyo
hataivumilia katika Wilaya yake na kuongeza kuwa kwa atakayebainika hatua kali
za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Picha na E. Kamanga
Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment