NDUGU wa marehemu Chambega Suwezi Buta (36) Mkazi wa Mkoa wa Tanga aliyefariki akiwa na madawa ya kulevya pipi 60 tumboni wamejitokeza kuja kuchukua mwili wa marehemu .
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alisema ndugu hao wamejitokeza juzi ofisini na kudai ya kuwa marehemu ni ndugu yao na hivyo wamekuja kufuata mwili huo ili kuusafirisha kwenda mkoani Tanga kwa mazishi.
Kamanda, alisema ndugu hao ambao hakuwataja majina walijitokeza juzi na kuchukuliwa maelezo , alama za vidole pamoja na kupigwa picha kwa ajili ya tahadhari hapo baadaye kabla ya kukabidhiwa mwili huo.
Akielezea tukio hilo Nyombi alisema, marehemu Chambega alifariki Desemba 3, mwaka huu akiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya ijulikanayo kwa jina la High Class iliyopo Tunduma Wilayani Mbozi chumba namba 108.
Alisema, Chambega alikuwa akitokea Tanzania kuelekea Afrika ya Kusini hivyo Tunduma alikuwa amejipumzisha kwa muda ili aweze kuendelea na safari yake ndipo pipi moja kati ya 60 alizokuwa amezimeza tumboni ilifunguka na kupelekea kifo chake.
Nyombi, alisema awali polisi walichukua mwili huo na kuupeleka hospitali ya wilaya ambapo mwili huo ukiwa umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti, ndipo askari kupitia uchunguzi wao walibaini kuwa marehemu alikuwa amehifadhi madawa ya kulevya tumboni.
Alisema, ndipo walipochukua mwili huo Desemba 6 mwaka huu na kuupeleka hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya upasuaji na kufanikiwa kukuta pipi 60 zikiwa tumboni ambapo 59 zikiwa nzima na moja ikiwa imefunguka.
Aidha, Kamanda Nyombi alisema pipi hizo zinazosemekana ni madawa ya kulevya zimepelekwa kwenye ofisi ya mkemia mkuu wa serikali ili kuzitambua kuwa ni aiana gani ya madawa ya kulevya.
Hata hivyo alisema uchunguzi zaidi unafanyika kujua mtandao mzima wa madawa ya kulevya kwani kuna tabia ya watu wenye fedha hupenda kuwatumia vijana wenye kipato kidogo kusafirisha madawa ya kulevya.
No comments:
Post a Comment