Naibu Waziri wa Afya na ustawi wa jamii, Dk.
Steven Kebwe akimpa pole mtoto Baraka Cosmas(6) aliyelazwa Hospitali ya
Rufaa kanda ya Mbeya baada ya kukatwa kiganja na watu wasiojulikana.
|
NAIBU waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.
Steven Kebwe amemtembelea mtoto Baraka Cosmas(6) mwenye ulemavu wa ngozi(albino)
aliyelazwa katika hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya baada ya kukatwa kiganja
cha mkono wa kulia na watu wasiofahamika.
Akiwa katika Wodi ya Watoto alikolazwa mtoto
huyo, Dk. Kebwe alisema ni vizuri akaanza shule mara baada ya kupona jeraha lake
ili aweze kuzoea kutumia mkono wa kushoto baada ya mkono wa kulia kuondolewa
kiganja ambapo hivi sasa hali yake inaendelea vizuri.
Naibu waziri huyo alisema kwa umri alionao
Baraka alipaswa kuanza shule hivyo akasisitiza kuwa ni muhimu mara tu baada ya
kupona jeraha lake akapelekwa shule akiwa katika mazingira yatakayoandaliwa
kiusalama kwake na kwa walemavu wengine wa ngozi.
Alisema kukosa kiganja cha kulia si sababu ya
mtoto huyo kukosa elimu kwakuwa kutokana na umri wake mdogo bado anaweza kusaidiwa
kuanza kutumia mkono wake wa kushoto katika shughuli mbalimbali ikiwemo masomo.
Aidha naibu waziri huyo alisisitiza waganga wa
jadi wanaopotosha umma kuendelea kufichuliwa na jamii huku pia akizitaka
halmashauri zilizochelewa kuondoa mabango ya waganga wa jadi kufanya hivyo
haraka.
Dk.Kebwe alisema suala la mapambano dhidi ya
ukatili unaofanywa kwa watu wenye ualbino ni la kila mwana jamii hivyo hakuna
mtu anayepaswa kulifumbia macho badala ya kutoa ushirikiano wa dhati.
Alisema serikali bado inaendelea na mikakati
madhubuti itakayowaweka watu wenye ulemavu huo kwenye mazingira salama sambamba
na kuwawajibisha watu wote watakaobainika kuhusika na vitendendo vya ukataji wa
viungo ama mauaji ya watu hao.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment