Mkurugenzi Idara ya Probesheni na huduma kwa jamii Wizara ya mambo ya ndani ya Nchi, Fidelis Mboya akimkaribisha mgeni rasmi |
Mratibu, Mradi wa Kuboresha Mafunzo ya Urekebishaji wa Wahalifu, Bw. Charles Nsanze |
Mahakimu na Maafisa Probesheni wa Mkoa wa Mbeya wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi |
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mkoa
wa Mbeya Mhe. Michael Mteite akimshukuru mgeni rasmi mara baada ya kufungua mafunzo kuhusu utekelezaji wa sheria za adhabu mbadala
|
Picha ya pamoja |
WATEKELEZAJI wa Sheria nchini wametakiwa
kupatiwa orodha ya aina mbalimbali za adhabu ili wazitumie katika
kuhukumu kulingana na mahitaji ya kila mkosaji ili hatimaye malengo ya adhabu
hiyo yatimie.
Maagizo hayo yalitolewa na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa
mbeya, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi, alipokuwa
akifungua mafunzo ya Mahakimu na Maafisa Probesheni wa Mkoa wa Mbeya
kuhusu utekelezaji wa sheria za adhabu mbadala,yaliyofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Mkapa, jijini Mbeya.
Dk. Nchimbi alisema Msongamano wa
wafungwa magerezani ulisababisha mambo matatu makuu, ambayo ni
Gharama kubwa za uendeshaji wa magereza kuwa mzigo mkubwa kwa serikali na hivyo
kusababisha hali duni ya maisha ya wafungwa kwa huduma za chakula na afya
jambo ambalo ni uvunjifu wa Haki za Binadamu kwa wafungwa.
Alisema jambo la pili ni Kuzorota kwa
utekelezaji wa jukumu la msingi la magereza la kuwarekebisha wakosaji na hivyo
kupelekea kuongezeka kwa viwango vya urudiaji wa uhalifu miongoni mwa wale
wanaomaliza kutumikia adhabu zao za jinai.
Aliongeza kuwa jambo la tatu Wahalifu wa makosa
madogo madogo kupelekwa magerezani kuchanganyika na wahalifu sugu na hivyo
kujifunza uhalifu mkubwa zaidi.
Alisema kutokana na hali hiyo kujitokeza, dunia
katika ngazi ya Umoja wa Mataifa iliandaa Sheria na Miongozo mbalimbali ambavyo
kwa ujumla wake vinasisitiza Adhabu Mbadala wa Kifungo Gerezani zitumike pale
inapostahili ili kuepukana na utegemezi uliokithiri wa Adhabu ya Kifungo
Gerezani.
Alizitaja adhabu hizo mbadala ni pamoja na
Faini, Onyo, Probesheni, Parole, Kifungo cha Nje, Huduma kwa Jamii, Kuachiliwa
kwa Masharti, Kuchapwa Viboko na nyinginezo nyingi tu ambazo zinatumika katika
nchi mbalimbali duniani.
Aliongeza kuwa malengo makuu ya kuwapa
adhabu wakosaji ni kuonya, kurekebisha, kutoa haki na kukinga au kulinda jamii
dhidi ya kosa au makosa yaliyotendwa.
Alisema ni jambo la muhimu kwa
watekelezaji wa Sheria kupatiwa orodha ya aina mbalimbali za adhabu ili
wazitumie katika kuhukumu kulingana na mahitaji ya kila mkosaji ili hatimaye
malengo ya adhabu hiyo yatimie.
“ Ni dhahiri kwamba kila mkosaji anapaswa
kuadhibiwa kulingana na tabia na mwenendo wake katika jamiii, mazingira ya kosa
lake, uzoefu wake wa makosa na hata umri na sababu za utendaji wake wa kosa”
alisema Dk Nchimbi.
Awali akimkaribisha Kaimu Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Idara ya
Probesheni na huduma kwa jamii Wizara ya mambo ya ndani ya Nchi, Fidelis Mboya,
alisema mafunzo hayo yamelenga kwa Mahakimu wote wa Mkoa wa Mbeya, Njombe na
Iringa, ambao wako katika ngazi za Hakimu Mkazi Mfawidhi, Hakimu Mkazi, Hakimu
wa mahakama ya Wilaya,Hakimu wa Mahakama za Mwanzo pamoja na Maprobesheni.
Alisema Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi mkubwa unaoendeshwa katika
nchi tatu za Afrika mashariki zikiwemo Tanzania, Uganda na Kenya ili kuboresha
adhabu mbadala kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza.
Alisema kutokana na ufinyu wa fedha kila nchi ilitakiwa kuchagua
Mkoa mmoja ambao mradi huo utatekelezwa ambapo kwa Tanzania Mkoa wa Mbeya ndiyo
ulipendekezwa na kuanza kutekelezwa kwa kutoa mafunzo mbali mbali kwa wadau.
Aliongeza kuwa mradi huo ni wa miaka miwili 2015 na 2016 ambapo
tayari mafunzo yalishafanyika kwa waandishi wa habari na kufuatiwa na Mahakimu
kisha kumalizia na wasimamizi wa vyombo vinavyosimamia wahalifu wanaotumikia
adhabu mbadala.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment