HATIMAYE
Serikali wilayani Chunya imeruhusu uvuvi katika Ziwa Rukwa kwa kipindi cha
Miezi mitano baada ya kufungwa kwa miezi sita iliyopita kutokana na kupungua
kwa samaki.
Uvuvi
katika ziwa hilo umeruhusiwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu hadi Desemba 31 mwaka
huu Ziwa litakapofungwa tena ili kuongezeka kwa samaki kuzaliana.
Sherehe
za uzinduzi huo zilifanyika juzi katika Forodha ya Mbagala Kata ya Mbangala
iliyopo Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Afisa Tarafa
ya Kiwanja, Shila Sheyo, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Chunya
Deodatus Kinawiro.
Afisa
Tarafa ya Kiwanja, Shila Sheyo, alisema zoezi la kufunga ziwa hilo litakuwa
endelevu ili kuwafanya samaki wazaliane na kuleta tija kwa wavuvi na uchumi kwa
wananchi wanaolizunguka ziwa Rukwa.
Alisema
kufungwa kwa Ziwa hilo kunatokana na wananchi kuvua bila utaratibu
kwa kutumia nyavu za makokolo na vyandarua hali inayosababisha kuharibu
mazalia ya samaki.
Alisema
kitendo cha kuruhusu shughuli za uvuvi hakumaanishi kuhalilisha kwa uvuvi
haramu kwani Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria kwa watu wote
watakaokiuka utaratibu.
Naye
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya,Julius Ngwita, ambaye pia
ni Afisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya, alisema Forodha ya Mbangala ndiyo
itakayotumika kupokelea Maboti na Mitumbwi kutoka maeneo yote ya wilaya ya
Chunya kwani hapo ndiyo katikati ambapo Serikali imejenga nyumba ya Afisa Uvuvi
Kanda iliyogharimu zaidi ya shingi milioni sitini zilizotolewa na Serikali.
Alisema
kila Mvuvi atatakiwa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kukata leseni ya
biashara,uchuuzi na vyombo vya majini kama mitumbwi na Maboti ili kuhakikisha
Serikali inapata mapato.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Mbangala,Abraham Sambila,mbali na kuipongeza
serikali kuruhusu kutumika kwa forodha hiyo na kuahidi kusimamia ipasavyo ili
kudhibiti mapato yatokanayo na shughuli hizo.
Alisema
fedha zitakazopatikana hapo zitasaidia kuleta maendeleo katika Kata yake na
Serikali kwa ujumla ambapo pia aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za
serikali.
Aidha
ameutaka uongozi wa Kijiji kupima viwanja kwa utaratibu na wananchi wanufaike
na mapato hayo ya mauzo ya viwanja na kuongeza mapato ya kijiji na
Halmashauri ya Wilaya kutokana na viwanja hivyo badala ya kugawa
kiholela.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment