IKIWA zimabakia siku chache kuanza kwa
shughuli za maonesho ya sikukuu za wakulima nane nane zinazotarajia kuanza
Agosti Mosi Mwaka huu kanda ya Nyanda za juu kusini lakini bado maandalizi yake
yanasuasua.
Maonesha hayo ambayo hufanyika kila
mwaka katika viwanja vya John Mwakangale Uyole jijini Mbeya huandaliwa na Chama
cha Wakulima Tanzania (TASO).
Akizungumzia maandalizi ya mwaka
huu, Katibu wa TASO kanda ya Nyanda za juu kusini, Ramadhani Kiboko,
alikiri kusuasua kwa maandalizi ya sikukuu za wakulima nanenane mwaka huu
tofauti na miaka iliyopita.
Kiboko alisema kawaida kila mwaka
maandalizi na shamla shamla za washiriki kuanza kuandaa maeneo yao pamoja na
vipando huanza Juni 30 lakini hadi sasa hakuna kinachofanyika pamoja na
jitihada za kuanza kutumika kwa stendi mpya.
Alisema tangu mwezi Machi mwaka huu TASO
ilitoa barua za mialiko ya kushiriki maonesho ya mwaka huu kwa washiriki 399
ambao ni pamoja na Halmashauri za Kanda, Taasisi za Serikali, bodi za mazao,
Taasisi za majeshi,Wizara za Serikali na vituo vya utafiti.
Alisema lakini katika watu wote hao
walioalikwa ni washiriki 298 waliothibitisha kushiriki kwa maandishi na wengine
kwa kukarabati maeneo watakayoyatumia pamoja na kuboresha vipando vyao.
Aidha Katibu alitoa wito kwa waalikwa
wengine ambao bado hawajajibu kama watashiriki kufanya hivyo mapema na kuanza
kufanya maandalizi tayari kwa maonesho yatakayoanza Agosti Mosi Mwaka huu.
Aliongeza kuwa kuna wengine ni wageni
hawajawahi kushiriki maonesho hivyo ni nafasi yao kuwahi ili waweze kuoneshwa
maeneo na kuanza maandalizi ya vitu wanavyotarajia kuvifanya wakati wa sherehe
hizo.
Pia alitoa wito kwa wafanyabiashara
mbali mbali kutumia Uwanja wa John Mwakangale katika biashara zao kwa
kuendeshea magulio au minada ya bidhaa mbali mbali kipindi ambacho kunakuwa
hakuna maonesho.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment