TIMU za Tanzania Prison na Mbeya City zote za jijini Mbeya zinatarajia kupimana nguvu katika mtanange utakaopigwa jumamosi hii(Julai 5, mwaka huu) kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine mjini hapa.
Aidha mchezo huo wa kirafiki pia ni maalumu kwa ajili ya majaribio ya mfumo mpya wa kielektroniki wa mashabiki kuingia uwanjani kwa kulipia tiketi zao kupitia mitambo maalumu iliyofungwa katika Uwanja huo na baadhi ya viwanja vitakavyotumika katika msimu ujao wa ligi kuu.
Hayo yalibainishwa jana katika Semina elekezi iliyotolewa kwa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya na viongozi wa mpira wa miguu iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu(TFF) ikiongozwa na Msemaji wake Bonifasi Wambura iliyofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine.
Akizungumza katika Semina hiyo Mwezeshaji ambaye ni mtaalamu wa mitambo hiyo kutoka benki ya CRDB, Kurrington Chahe, alisema tiketi za mchezo huo zilianza kuuzwa siku tano kabla na ndivyo itakavyokuwa katika michezo yote ya ligi kuu.
Alisema lengo ni kumfanya shabiki kununua tiketi popote alipo hapa nchini kutokana na mfumo huo kufanyika kwa nia ya mtandao ambapo shabiki anaweza akanunua kwa njia ya mitandao ya simu ama kufika katika tawi la Benki ya CRDB.
Aliongeza kuwa lengo la kufunga mashine hizo ni kudhibiti mapato ya uwanjani ambapo fedha zote zitakuwa zikipitia moja kwa moja benki na kwa mawakala na sio mikononi mwa watu kama ilivyokuwa awali.
Alisema kutumika kwa mfumo huo pia kutaondoa wanaojiita stafu ili wapiti bure pamoja na makomandoo wa timu wanaokaa milangoni na kuingiza watu bure.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TFF, Bonifasi Wambura alisema mfumo huo ni mpya na unaweza ukawa na changamoto nyingi ndiyo maana wameandaa mechi ya kirafiki baina ya Mbeya city na Tanzania Prison ili kujaribu matumizi ya mitambo hiyo.
Alisema kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa shilingi 3000 ambapo shabiki atafika na tiketi yake getini ambayo itaskaniwa kwenye mashine ili kubaini idadi ya watu wakaoingia uwanjani pamoja na mapato yake ambapo alisema utaratibu huo utaondoa usumbufu wa kuanza kuhesabu mapato baada ya mechi.
Wambura alisema tiketi zitasitishwa kuuzwa katika kipindi cha pili cha mchezo kinapoanza ili kuweza kurahisisha utaratibu mwingine kufanyika ambapo aliongeza kuwa mfumo huo utapunguza gharama nyingi zikiwemo magari ya kuuzia tiketi.
Katika mchezo huo Mawakala zaidi ya 15 wamefundishwa na kuteuliwa kuuza tiketi hizo kutoka Wilaya za Mkoa wa Mbeya na jijini hapa.
No comments:
Post a Comment