Mwenyekiti wa Kamati ya Marafiki wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Oleais Senga, ambao walijitolea kuchangisha fedha za ujenzi wa njia za kupitishia wagonjwa.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya,Dk. Grolia Mbwile, akionesha sehemu ambazo njia hiyo itajengwa .
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya,Dk. Grolia Mbwile akionesha ramani ya ujenzi huo
WADAU wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya wameombwa michango yao ya hali na mali ili kufanikisha ujenzi wa njia za kupitia wagonjwa katika Hospitali hiyo ujenzi unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi Milioni 240.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Marafiki wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Oleais Senga, ambao wamefanikisha kuandaa harambee ya kukusanya fedha za kufanikisha ujenzi huo ambapo katika Harambee hiyo zilipatikana Ahadi za fedha zaidi ya shilingi Milion 80.
Senga alisema baada ya hapo wadau mbali mbali wameendelea kutimiza ahadi zao ambapo hadi sasa wameshakusanya zaidi ya Shilingi Milion 40, hivyo ametoa wito kwa waliobaki kukamilisha ahadi zao ili kufanikisha ujenzi huo ili kuwakomboa wagonjwa.
Aliongeza kuwa wakati fedha zingine zikisubiriwa kukamilishwa kwa walioahidi ni vema wadau wengine wakajitokeza kuchangia fedha zilizosalia ili kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya kupitishia wagonjwa kwa njia ya vitanda vyenye magurudumu.
Hata hivyo alisema fedha hizo kidogo zilizopatikana zitaanza kufanya kazi kesho baada ya kumpata mkandarasi aliyekubali tenda hiyo ya bila malipo ambapo Kamati itatakiwa kununua vifaa na kuwalipa mafundi pamoja na vibarua.
Alimtaja Mkandarasi huyo kuwa ni Inter Frempa Co.Ltd yenye makao makuu jijini Mbeya pamoja na Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia(MUST) waliojitolea kuchora ramani ya ujenzi huo bure bila malipo yoyote.
Alisema kujitolea kwa watu hao kumepunguza baadhi ya gharama na kurahisisha ujenzi na kutoa wito kwa wadau kujitoa kwa hali na mali ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati kupitiaMpesa 0762 321829 yenye jina la Marafiki Mkoa au akaunti namba 0150067027600 CRDB jina Marafiki wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hosipitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Grolia Mbwile, mbali na kuipongeza kamati hiyo pamoja na chuo cha MUST na Mkandarasi aliyejitolea alitoa wito kwa wananchi mbali mbali wenye uwezo wa kuchanga chochote akafanya hivyo ili kufanikisha ujenzi huo.
Alisema sio lazima mtu akatoa fedha bali anaweza kujitolea Mchanga, Kokoto, Sementi, Misumari,Mbao, Vyuma na mabati ambavyo kwa namna moja ama nyingine vitarahisisha matumizi ya fedha kupungua.
Naye Mkandarasi atakayesimamia Ujenzi huo, Mhandisi Wilson Mwangonela alisema endapo fedha zote zinazohitajika ambazo ni Shilingi 240,877,575 zitakuwepo zote ujenzi huo unaweza kukamilika ndani ya Wiki tatu hadi nne.
Na Mbeya Yetu
No comments:
Post a Comment