LIGI ya mpira wa miguu ya Kombe la Boda
boda 2014 lililokuwa linatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 10, Mwaka huu
limesogezwa mbele hadi Juni 14, Mwaka huu kutokana na mwingiliano wa ratiba na
ligi zingine.
Akizungumza katika mkutano na waandishi
wa habari uliofanyika kwenye viwanja vya City Pub jijini Mbeya, Meneja wa
Matukio wa kampuni ya Citysign Promotion & Marketing agency, Geophrey
Mwangunguru, ambao ndiyo wandaaji wa ligi hiyo alisema mbali na mwingiliano wa
ratiba pia ni maombi ya mdhamini mkuu.
Mwangunguru alisema hivi sasa michuano
hiyo imepata mdhamini mkuu ambaye ni kampuni ya vinywaji ya Cocacola kwanza
Kanda ya Mbeya hivyo kuomba michuano hiyo kusogeza mbele kutokana na kuwepo kwa
ligi nyingine ya Mastala cup ambayo inaanza Mei 10, Mwaka huu na kudhaminiwa na
Cocacola.
Alisema mdhamini ameona ni vema ligi
hizo zikapishana ili kuleta mvuto kwa jamii na kutoa burudani mfululizo kwa
wapenzi wa mpira wa miguu katika Jiji la Mbeya kwa kutofautisha ratiba.
Kwa upande wake Meneja masoko na mauzo
wa Cocacola Mbeya, Jayant Vekaria alisema wanajisikia faraja kutoa udhamini kwa
kundi maalumu kama madetreva wa bodaboda ambayo wamekuwa wakisemwa vibaya
mitaani.
Alisema jamii inapaswa kuelewa kuwa
madereva wa bodaboda wamejiajiri sawa na ajira zingine hivyo waheshimiwe na
kupitia ligi hiyo ndipo jamii itakapowatambua kuwa nao ni raia wema kama
walivyo wengine.
Aliongeza kuwa Kampuni yao imeguswa na
kundi hilo hivyo kuamua kutoa udhamini mnono unaofikia Shilingi Milioni
14.2 ambazo zitasaidia kuandaa mashindano pamoja na zawadi kwa washindi
katika nafasi tofauti tofauti na kwamba ligi hiyo itaitwa Cocacola Bodaboda cup
2014.
Alizitaja zawadi hizo kuwa ni mshindi wa
kwanza kujinyakulia Pikipiki mpya moja, mshindi wa Pili fedha taslimu shilingi
Laki saba, mshindi wa tatu shilingi laki tatu huku mfungaji bora, timu yenye
nidhamu uwanjani na Golikipa bora wakiambulia shilingi laki moja kila mmoja.
Mbali na kuahirishwa kwa ligi hiyo timu
zilizothibitisha kushiriki ligi hiyo zilikabidhiwa vifaa vya michezo
ikiwemo mipira na jezi kutoka kwa wadhamini ambao ni kampuni ya Cocacola,
Kihumbe na Nwaka Mwakisu ambaye pia ni mlezi wa Chama cha madereva wa bodaboda Mkoa
wa Mbeya.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment