KATIKA
hali isiyokuwa ya kawaida Mwanamke mmoja Mkazi wa Mtaa wa Ilembo kata ya
Iyela Jijini Mbeya amemjeruhi mume wake baada ya kumwagia mafuta ya moto
kichwani kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mgogoro wa ndoa baina yao.
Mwanamke
huyo aliyefahamika kwa jina la Beatrice Lusamba (37) alitenda tukio hilo
mwishoni mwa wiki majira ya saa saba mchana ambapo alimwagia mafuta hayo Mume
wake Lugano Mwambuja(50) ambaye ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Sange iliyopo
Wilaya ya Ileje Mkoani Mbeya.
Akizungumzia
tukio hilo Mhanga wa kisa hicho alisema yeye makazi yake yako Wilayani Ileje
lakini Mkewe pamoja na baadhi ya watoto wake huishi Jijini Mbeya hivyo hufika
nyumbani hapo mara chache kwa ajili ya kutembelea familia na kupeleka huduma
mbali mbali kama baba wa familia.
alisema
siku ya tukio alialikwa na Mkewe huyo kula chakula cha mchana ambapo baada ya
kukaribishwa ndani mwanamke huyo aliingia jikoni akiwa na mayai matatu na
galoni la mafuta ya kupikia, ambapo yeye alibaki Sebureni akisubiri chakula
alichokaribishwa apikiwe.
Alisema
baada ya dakika kumi Mkewe huyo alirejea Sebuleni akiwa ameshika kikombe chenye
mafuta yaliyochemshwa ambayo alimwagia mwilini na kisha kukimbilia nje
akimwacha mumewe akiugulia maumivu makali yaliyotokana na kuungua na mafuta ya
moto mwilini mwake.
Mwalimu
huyo aliongeza kuwa baada ya kupiga kelele ya kuomba msaada ndipo alipojitokeza
jirani yake aliyefahamika kwa jina la Andamisye Kajange ambaye baada ya kumuona
katika hali hiyo alimkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya alikopatiwa
matibabu na kuruhusiwa.
Mjumbe
wa Mtaa Ilembo, Philly Mwakapimba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kuongeza kuwa kabla ya kupeleka Hospitali Mhanga waliripoti Kituo cha Polisi na
kupewa fomu namba tatu (PF3) pamoja na kufungua faili namba IR/2253/2014
na kuendelea kutibiwa.
Aliongeza
kuwa mtuhumiwa hajakamatwa hadi leo baada ya kutorokea kusikojulikana huku
lawama likipewa Jeshi la Polisi kutokana na kushindwa kumkamata mtuhumiwa kwa
wakati hadi anapata mwanya wa kutoweka katika eneo la tukio.
Akizungumzia
mahusiano yake na mkewe Mwalimu huyo alisema alioana na mkewe mwaka 2007 kwa
ndoa ya kimila baada ya kufiwa na mkewe wa awali mwaka 2006 alimyemwachia
watoto wawili ambao ni Doris(20) na Happy Mwambuja(21) ambapo aliamua kuoa mke
huyo kwa ajili ya kusaidia malezi ya watoto hao.
Alisema
akiwa kazini mara nyingi alikuwa akipata taarifa za mgogoro kati ya mkewe huyo
na watoto jambo lililosababisha usuluhishi wa mara kwa mara kufanyika
ukiongozwa na Serikali ya Mtaa huku sababu ikibainika kuwa ni tamaa ya mwanamke
huyo kutaka kumiliki Nyumba ya Mwalimu huyo ili iwe mikononi mwake na siyo
Familia.
Alisema
mara nyingi Mwanamke huyo amekuwa akijaribu kuiba hati ya nyumba ili abadilishe
majina na umiliki lakini anashindwa hali iliyoml;azimu Mwalimu huyo kuamua
kununua eneo lingine na kujenga ili kumtengnisha mkewe pamoja na watoto lakini
hali bado ilikuwa tete baada ya mwanamke huyo kutaka amilikishwe yeye nyumba.
hadi
sasa Mwalimu huyo anaendelea kupatiwa matibabu Nyumbani kwake huku Jeshi la
Polisi likiendelea kumsaka mtuhumiwa kwa ajili ya kumfikisha katika vyombo vya
sheria kujibu shtaka la kujeruhi kwa makusudi.
mwisho.
Na Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment