HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, imewafukuza kazi maafisa watendaji saba kwa makosa mbalimbali likiwemo la ubadhilifu wa mali ya umma na utoro kazini.
Tamko la kuwafukuza kazi watendaji hao limetolewa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Jiji la Mbeya kilichofanyika hivi karibuni, ambapo baraza hilo liliridhia kufukuzwa kwa watendaji hao.
Mkurugenzi wa jiji la Mbeya, Juma Rashid Idd aliwataja watendaji hao kuwa ni Laston Kaselama afisa mtendaji wa mtaa wa Mbata ambaye alihusika na wizi wa fedha zaidi ya milioni 9, Venance Mlozi afisa mtendaji mtaa wa Tembela kwa kosa la utoro kazini.
Aliwataja wengine kuwa ni Hussen Kelaza afisa mtendaji mtaa wa Iganjo, Wase Claus afisa mtendaji mtaa wa Mbeya Peack, Yunis Msomba afisa mtendaji mtaa wa Mwamfute na Kristopher Mashambo afisa mtendaji mtaa wa Ilolo ambao wote walikuwa na kosa la utoro kazini na kutorudisha kitabu cha mapato na matumizi.
Mkurugenzi Juma alimtaja afisa mtendaji wa Kata ya Iwambi Zuhura Mustafa kwamba alikuwa anakabiliwa na kosa la wizi wa pembejeo za mbolea ya ruzuku pamoja na kutorudisha kitabu za mapato na matumizi.
Majina ya watuhumiwa wote saba yalifikishwa kwenye Kamati ya maadili na kujadiliwa na kisha kuyafikisha kwenye baraza ili kulidhia ikiwa na kutoa tamko.
Aidha, baraza hilo ambalo lilikaa kikao chake lilidhia mashauri hayo na kuyatolea tamko la kufukuzwa kazi kwa watendaji hao.
|
No comments:
Post a Comment