Ofisi za Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya zimenusurika kuchomwa moto baada ya kumwagiwa Petroli na watu watatu wanaodaiwa kutumwa kuteketeza nyaraka zilizokuwemo katika ofisi hizo.
Watu hao watatu wanaodaiwa kutumwa na mmoja wa wafanyabiashara wa eneo la Rujewa walifika katika ofisi hizo majira saa 8.00 usiku wa kuamkia jana, ambapo walimwagia mafuta aina ya petroli katika ofisi hizo na mara mlinzi wa ofisi hizo akagundua na hatimaye alipiga risasi mbili ambayo moja ilimpata begani na alipojaribu kukimbia risasi ya pili alipigwa mguuni eneo la goti na wawili kufanikiwa kukimbia.
Habari zaidi zinadai kuwa watu hao ni wakazi wa Makambako - Njombe ambapo walitumwa na mfanyabiashara aliyetambulika kwa jina la Eppymark Shayo mfanyabiashara kutoka Rujewa ambaye ndiye aliyekwenda kuwachukua watuhumiwa hao ambao ni Alex Nombo, Jemi Makweta na Mwamengele Makweta.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ancletius Malindisa alipohojiwa kuhusu tukio hilo alikiri kutokea na kwamba tayari jeshi la polisi Mkoa hapa linawashikiliwa watu wawili kuhusiana na tukio hilo.
Aliwataja wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo kuwa ni pamoja na Alex Nombo (20) mkazi wa Igando katika mji wa Makambako ambaye ndiye alijeruhiwa begani na mguuni kwa risasi baada ya wenzie wawili kukimbia na kutokomea kusikojulikana .
Alisema kuwa kijana huyo ameshatolewa katika hospitali ya mission ya Chimala na jana jioni alihamishiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya matibabu zaidi, ikiwa ni kufanyiwa upasuaji kuziondoa risasi zilizokuwa mwilini huku akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la Polisi.
Alimtaja mwingine aliyekamtwa kuwa ni mfanyabiashara anayedaiwa kuwatuma vijana hao aliyetambulika kwa jina la Eppymark Shayo Mkazi wa Rujewa Wilayani Mbarali ambaye anashikiliwa katika kituo Kikuu cha Polisi cha kati baada ya kukamatwa eneo la Mwanjelwa jijini Mbeya.
Kamanda wa Takukuru Wilaya ya Mbarali Ramandan Ndwata amesema kuwa hawezi kutoa taarifa kwasababu tukio lenyewe ni nyeti linahitaji uchunguzi wa kina zaidi.
Kwa upande wake kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mbeya Daniel Mtuka amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba taasisi yake imejipanga vilivyo na haiteteleki na itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na kamwe haitamwachia mtu yeyote anayejihusisha na Rushwa ya aina yeyote.
No comments:
Post a Comment