Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Monday, August 1, 2011

Wauguzi KCMC, Mawenzi wahojiwa kwa mauaji

Daniel Mjema, Moshi
WAUGUZI wawili, mmoja wa Hospitali ya Rufaa KCMC na mwingine wa Hospitali ya Mkoa Kilimanjaro, Mawenzi, wanahojiwa na polisi kwa tuhuma za kula njama na kupanga mauaji ya msichana mmoja, mkazi wa Kibosho.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana, zilisema ingawa mauaji hayo yanaaminika kutokea kati ya Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu, lakini siri ya mauaji hayo imefichuka Julai mwaka huu.

Taarifa hizo zilidai, polisi wamekwishaandikia ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kufanya taratibu za kisheria kufukuliwa kwa miili ya wanawake watatu ili ifanyiwe vipimo vya vinasaba (DNA), kuwatambua.

Polisi wanaamini moja ya maiti hizo zilizookotwa maeneo tofauti Wilaya ya Moshi na Hai, inashukiwa ni ya mwanamke aitwaye Rufina Joseph, ambaye ametoweka miezi saba sasa. Maiti hizo zilizikwa na manispaa kwa kukosa ndugu.Wauguzi hao wawili walikamatwa Julai 6, mwaka huu na kuwekwa mahabusu kwa wiki moja hadi Julai 13, walipoachiwa kwa dhamana licha ya kesi za mauaji kutokuwa na dhamana hata kama iko hatua za awali za uchunguzi.

Chanzo kimoja kilidokeza kuwa, siri ya mauaji hayo ilifichuliwa na dereva teksi mmoja ambaye alifahamu mipango yote ya suala hilo, ambalo sasa linawaumiza vichwa wapelelezi wa polisi.

Sakata lilianza mwanzoni mwa mwaka 2010
Taarifa za uhakika zilisema mmoja wa washukiwa ambaye ni muuguzi Idara ya Utabibu KCMC (jina tunalo), alipata ‘dili’ ya Wazungu waliokuwa tayari kumtumia fedha, lakini sharti likiwa ni kuthibitisha kuwa na mtoto mchanga.
Kwa kuwa muuguzi huyo alikuwa hawezi kupata mtoto, alianza harakati za kutafuta mtoto mchanga hata ikibidi wa kununua na mipango hiyo akimshirikisha rafiki yake, ambaye ni muuguzi wa Wodi ya Wazazi Hospitali ya Mawenzi.

Wauguzi hao inadaiwa walikwenda kuzungumza na wazazi ambao walikuwa na watoto wachanga maeneo ya Uchira na Uru Moshi Vijijini, ikiwamo mama mmoja aliyekuwa amejifungua watoto mapacha, lakini waligoma kumpa mtoto.
Katika kuhangaika huku na kule bila mafanikio, muuguzi huyo wa KCMC akishirikiana na dereva teksi aliyemwajiri, walipata taarifa kuwa yuko msichana mwenye mimba ya miezi minane eneo la Kibosho.

“Kwa hiyo yule muuguzi wa KCMC naye akawaarifu watumishi wenzake kuwa, ana mimba ya miezi minane sambamba na ya yule dada wa Kibosho, ili atakaposingizia amejifungua ifanane na yule wa Kibosho,” kimedokeza chanzo chetu.
Msichana huyo alipata mimba hiyo kwa bahati mbaya na wazazi wake walikuwa wakigombeza kutaja mhusika, ili aweze kubeba gharama za matunzo. hivyo kitendo cha kupata msamaria kilimpa faraja.

Inadaiwa wauguzi hao kwa kushirikiana na dereva teksi huyo walimghilibu dada huyo ambaye alikuwa njiapanda na kukubaliana kuwa baada ya kujifungua, muuguzi wa KCMC angemchukua mtoto na kumsaidia kumlea.
Baada ya makubaliano hayo, muuguzi huyo wa KCMC aliwaarifu wafanyakazi wenzake kuwa ni mjamzito mwenye mimba ya miezi minane na kwamba anakaribia kujifungua lakini asingejifungulia KCMC, bali Hospitali ya Kibosho.
Msichana huyo alijifungua Aprili mwaka jana kwa operesheni kwenye hospitali hiyo na kukaa siku nne, ndipo wauguzi hao walipoomba kwa maandishi aruhusiwe kurudi nyumbani.

Madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Kibosho walikubali ombi hilo na kukaa kwa siku moja kwa muuguzi wa Hospitali Mawenzi eneo la Soweto mjini Moshi, siku iliyofuata alihamishiwa nyumbani kwa yule wa KCMC.
Baada ya kufika huko na kukaa mwezi mmoja, muuguzi huyo wa KCMC alimshawishi msichana huyo kumwachia mtoto kwa ahadi kwamba akamtafutie kazi Dar es Salaam.

Inadaiwa kuwa mwanamke huyo alikubali na kumwacha mtoto wake mchanga kwa muuguzi huo wa KCMC, ili amsaidie kumlea na yeye kupelekwa Dar es Salaam ambako alitafutiwa kazi ya kuuza baa moja (jina la baa tunalo).

Katika kipindi chote hicho cha mwezi mmoja alichokaa na muuguzi huyo wa KCMC, mama wa mtoto alikuwa akitambulishwa kama mfanyakazi wa ndani.
Muuguzi KCMC alipongezwa kwa kujifungua salama
Wakati wote, muuguzi wa KCMC akawataarifu watumishi wenzake na majirani kuwa amefanikiwa kujifungua salama na kuwaonyesha mtoto na alipokea pongezi na zawadi kutoka sehemu mbalimbali.
Kubwa zaidi ni kuwa muuguzi huyo akaendelea kumnyonyesha mtoto kama wa kwake kuanzia Aprili hadi Desemba 2010, hakuna aliyeshuku kuwa mtoto huyo siyo wake.

Chanzo cha mgogoro wa mtoto
Desemba kama ilivyo ada kwa wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro, mama wa mtoto alirejea Moshi kwa ajili ya Sikukuu ya Krismas na mwaka mpya.Taarifa za polisi zilidai kuwa mama wa mtoto alifika nyumbani kwa muuguzi huyo na kumwomba ampatie mwanaye, ili kwenda naye Kibosho kwa bibi yake kumsalimia, lakini muuguzi alimbadilikia na kumweleza wazi kuwa hakuwa na mtoto pale, jambo lililomfanya kuamini kuwa pengine ni utani, kwani hakuamini angegeukwa kiasi hicho kwa damu yake.

Inadaiwa kitendo cha mama wa mtoto kushikilia msimamo wa kutaka kuondoka na mtoto wake, kilimweka njiapanda muuguzi yule wa KCMC akijiuliza jinsi ya kujieleza kwa wafanyakazi wenzake na jamii.
Taarifa hizo zinadai siku moja kabla ya mama wa mtoto kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, muuguzi yule wa KCMC na mama wa mtoto walionekana wakinywa pombe nyingi na vijana wasiofahamika mtaani walipokuwa wakiishi.

Kufichuka kwa siri ya mauaji
Kitendo cha muuguzi wa KCMC kuendelea kumnyonyesha mtoto yule licha ya taarifa za mama yake kurejea Moshi, kilimshitua dereva teksi ambayo alimhoji kulikoni, lakini muuguzi akamtaka kutofuatilia mambo ya watu.
Baada ya kuonekana akifuatilia sana huku akihoji alipo mama wa mtoto, muuguzi yule alimweleza dereva teksi kwamba amemtafutia kazi nyingine katika baa moja iliyopo Korogwe, mkoani Tanga.

Kutokana na mashaka aliyokuwa nayo, dereva yule alifuatilia hadi Tanga na kugundua kulikuwa hakuna baa yenye jina hilo alilotajiwa, ndipo alirejea Moshi na kumweleza muuguzi huyo kwamba baa aliyomtajia haipo.
Muuguzi yule alienda mbali na kumtaka dereva huyo kumkabidhi funguo za gari aliyokuwa akiendesha. Muuguzi huyo anamiliki teksi mbili.Kitendo hicho kinadaiwa kilimchukiza dereva yule ambaye baadaye aliamua kufichua siri ya tukio hilo kwa mama mzazi wa mtoto aitwaye, Magdalena Mwacha, ambaye baadaye alitoa taarifa polisi.

Mama mzazi asimulia mwanaye alivyotoweka
Akizungumza katika ofisi za Mwananchi Moshi wiki iliyopita, Magdalena alisema baada ya mwanaye kujifungua, alipewa taarifa na jirani yake kuwa asiende tena kumchukua Hospitali ya Kibosho kwani amechukuliwa na wauguzi hao.
“Nilisisitiza nataka nimwone mjukuu wangu, ndipo yule jirani aliponipeleka nyumbani kwa yule nurse (muuguzi) wa KCMC na kweli nilimkuta mjukuu wangu, lakini mwanangu sikumwona wakaniambia atarudi tu,” alisema na kuongeza:
”Baada ya kukaa hadi saa 12:30 jioni bila kumwona mwanangu, niliamua kurudi Kibosho lakini baada ya mwezi nilirudi kwa yule muuguzi na kumkuta akiwa na mjukuu wangu tu mama yake hakuwepo.”

Mama huyo alidai kuwa siku moja Desemba, mwanaye alimpigia simu kuwa angekuja likizo ya Krismas na siku aliyosafiri alimjulisha pia, lakini akamwambia kuwa angepitia mahali ingawa hakumwambia sehemu yenyewe.
“Baada ya kutomwona hadi Januari niliamua kutoa taarifa polisi, ambao waliwakamata wale wauguzi na kuandikisha maelezo yao na kuwaachia, huku wakiniambia niendelee kumtafuta mtoto wangu,” alisema.

Alisema Juni 29, mwaka huu alipokea simu kutoka kwa dereva teksi akimwambia aende kumwona ili wazungumze kuhusu kutoweka kwa mwanaye, aliitikia wito huo na kwenda Moshi mjini na kukutana na dereva huyo.
“Aliniambia kuwa Rufina alifika nyumbani kwa yule muuguzi wa KCMC Desemba akimtaka ampe mtoto wake, lakini alikataa na kumchukua na kwenda kumnyesha pombe na baadaye kukodisha watu wa kumuua,” alisema.

Kauli ya RPC Kilimanjaro
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absolom Mwakyoma, alilithibitishia kuhojiwa kwa wauguzi hao na dereva teksi mmoja na kwamba, hivi sasa wako nje kwa dhamana ya polisi.“Ni kweli hilo jambo hilo lipo, lazima tuthibitishe kama kweli huyo mwanamke ni marehemu ili sasa tuweze kuunganisha ushahidi tulionao, njia pekee ni kufanya vipimo vya DNA ili tusikurupuke,” alisema Mwakyoma.

Kwa mujibu wa Mwakyoma, zipo maiti za wanawake watatu zilizookotwa ambazo utaratibu unafanyika ili zifukuliwe na kufanyiwa vipimo vya DNA, ili kuthibitisha kama upo mwili wa mwanamke huyo aliyetoweka.'Kama tutathibitisha kuwa mwili ule ni wa Rufina, bado jukumu letu lingine litakuwa ni ku establish (kutafuta chanzo) kama sababu za kifo ili sasa tuweze kuunganisha hadithi hizo ulizozisikia,” alisema Mwakyoma.
Chanzo: Mwananchi
"

No comments: