TIMU ya taifa ya soka ya wanawake Tanzania ‘Twiga Stars’ ilianza vema michuano ya Shirikisho la Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) kwa kuichapa mabao 3-1 Botswana kwenye Uwanja wa Gwanzura jijini Harare, Zimbabwe.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kuvutia walioing’arisha ni Mwanahamis Omar ‘Gaucho’ aliyetupia nyavuni mabao mawili dakika ya tisa na 88 huku Fatuma Mustafa ‘Kitu Nini’ dakika ya 32.
Twiga iliyo kundi A katika michuano hiyo, kesho itaivaa Lesotho kwenye Uwanja wa Rufaro kabla ya kumaliza mechi za makundi Julai 5 dhidi ya wenyeji kwenye Uwanja wa Gwanzura.
Hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo itafanyika Julai 7, ambako kila kundi litatoa timu mbili kuingia katika hatua hiyo.
Twiga Stars inashiriki michuano hiyo kama mwalikwa, ambapo timu nane zinatarajiwa kushiriki, ambazo ni Zimbabwe, Lesotho, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Msumbiji na Malawi.
Habari kwa hisani ya Francis Godwin
No comments:
Post a Comment