Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ukosefu mkubwa wa ajira na nafasi za kujiendeleza kwa vijana wa Afrika ni bomu linalosubiri kulipuka na linalohitaji majawabu ya haraka kulizuia lisilipuke.
Rais Kikwete amesema kuwa ni wajibu na jukumu la viongozi wa Afrika kuwekeza ipasavyo katika vijana ili kuwawezesha kutimiza nafasi yao ya Kihistoria kwa sababu vijana ndio mhimili wa leo na kesho wa “familia , jamii zetu na mataifa yetu.”
Rais Kikwete ameyasema hayo Alhamisi, Juni 30, 2011, wakati alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa 17 wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) unaotarajiwa kumalizika Julai 01, 2011 katika Ukumbi wa AU wa Palace of Conferences katika kijiji cha kisasa cha Sipopo, nje kidogo ya mji mkuu wa Malabo, ulioko katika Kisiwa cha Bioko cha Equatorial Guinea.
Akichangia katika mjadala wa mada kuu ya Mkutano wa mwaka huu ya “Uharakishaji wa Uwezeshaji wa Vijana kwa Maendeleo Endelevu”, Rais Kikwete amependekeza njia kuu za kusaidia kupunguza tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na hata nafasi za kujiajiri kwa vijana wa Afrika.
“Afrika ni bara dogo kwa umri kwa sababu ya wakazi wake wengi ni vijana na ongezeko la watu kwenye Bara hili ni kubwa kuliko eneo jingine duniani. Lakini vijana wa Afrika wanakabiliwa na changamoto nyingi, kubwa kuliko zote ikiwa ni ukosefu wa ajira.
“Ni bomu ambalo likiachiwa bila kushughulikiwa ipasavyo, litakuwa chanzo kikubwa cha kuyumba kwa nchi zetu zote,” Rais Kikwete amewaambia viongozi wenzake na kuongeza:
“Mageuzi tuliyoyashuhudia katika nchi za Kiarabu yanaweza kuwa ni mwanzo tu. Vijana katika Afrika ni asilimia 37 ya watu wote walioajiriwa lakini bado vijana ni asilimia 60 ya watu wasiokuwa na kazi katika Bara letu. Sisi, wazazi, viongozi wa Serikali zao tuna wajibu maalum kwa vijana wetu. “
“Kwanza kabisa ni lazima tuhakikishe kuwa vijana wetu wanakua na kuwa watu wazima katika afya njema, tuhakikishe kuwa wanapata elimu bora na tufanikishe wapate ajira za heshima na zenye malipo mazuri. Siyo kazi rahisi lakini ni lazima tuifanye.”
Kuhusu nini kifanyike, Rais Kikwete kwa kutumia uzoefu wake wa kuwa mjumbe wa Tume ya Denmark-Afrika Kuhusu Ajira kwa Vijana Katika Afrika amesema kuwa hatua kubwa ambazo viongozi wa Afrika wanapaswa kuzichukua ni pamoja na kubuni sera nzuri za kisiasa, kiuchumi na kijamii ambazo zinaweza kusaidia kufungua uwezo mkubwa wa vijana wa Afrika.
Rais Kikwete amesema kuwa sera hizo zilenge kuchochea ukuaji mkubwa zaidi wa uchumi, ongezeko kubwa la uwekezaji katika uchumi wa Afrika, ongezeko la uwezo wa ushindani na kuzalishwa kwa nafasi nyingi zaidi za ajira kwa vijana.
“Tunahitaji kubuni sera mwafaka zitakazowawezesha vijana wetu kupata ujuzi ambao utawawezesha kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe; sera ambazo zitawawezesha kujipatia uwezo wa kuwa wazalishaji mali wa kuweza kuendesha biashara nzuri; sera ambazo zitachochea maendeleo ya sekta binafsi ili sekta hiyo iweze kuzalisha ajira kwa ajili ya vijana wetu, wasichana na wavulana,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye anashiriki Mkutano huo wa 17 wa AU anatarajiwa kuondoka mjini Malabo kuelekea nyumbani kesho, Jumamosi, Julai 02, 2011.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
Malabo, Equatorial Guinea.
01 Julai, 2011
No comments:
Post a Comment