Dereva John Gwau akiwa amelazwa wodi no.4 hospitali ya mkoa wa Singida akiendelea kupata matibabu baada ya kupigwa na shemeji yake Celestin Mgoo kwa tuhuma ya kufuliwa nguo na dada yake Ruth ambaye wametengana na Celestin.Picha na Gasper Andrew...
John Gwau akiwa Hospitalini akipatiwa matibabu.Picha na Gasper Andrew.
--
Na. Nathaniel Limu
Dereva wa kampuni ya usafirishaji ya ‘Rich On’ ya jijini Dar-es-salaam John Gwau (35) amenusurika kuuawa na shemeji yake baada ya kupigwa vibaya kichwani na chupa ya bia.
Akizungumza kwa taabu akiwa amelazwa wodi namba nne katika hospitali ya mkoa,Gwau amesema alikumbana na dhahama hiyo julai nne mwaka huu saa sita usiku eneo la Mughanga mjini humo.
Amesema mapema siku hiyo ya tukio,shemeji yake Celistin Mgoo ambaye ametengana na dada yake anayeitwa Ruth,alimgombeza Ruth kwa kitendo chake cha kufua nguo zake (Gwau).
Dereva huyo amesema Ruth alimjibu Celistin kuwa haoni kosa lo lote kwa kitendo cha kufua nguo za kaka yake Gwau ambaye kwa wakati huo,alikuwa mgonjwa.
“Majibu hayo na kitendo cha dada kufua nguo zangu,vilimuudhi shemeji ambaye usiku huo alinijia chumbani kwangu akiwa na chupa tano za bia kwa lengo la kuzitumia kunipiga”alisema.
Gwau amesema baada ya kuingia chumbani, alimpiga kichwani na chupa ya bia na kupelekea aanguke chini na kuzirai na kuzinduka kesho yake mchana.Baada ya kuzirai,mtuhumiwa alitumia chupa hiyo iliyopasuka kwa kumcharaga sehemu mbalimbali za uso.
“Dada yangu Ruth ambaye ni mwalimu katika shule ya msingi Mughanga na ndugu yangu Athumani Rajabu,baada ya kuniona natokwa damu nyingi huku nikiwa nimezirai,wote wawili walianguka chini na kuzirai.Wote wamelazwa hapa hospitali ya mkoa”alisema Gwau.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida,Celina Kaluba,amekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa Celestin amepandishwa kizimbani Julai5 ,2011) kujibu tuhuma inayomkabili.
No comments:
Post a Comment