Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Saturday, June 25, 2011

WABUNGE WASISITIZA PESA YA BAE SYSTEM ITATUMIWA KUENDELEZA ELIMU YA WATOTO TANZANIA…!!!





Naibu Spika Wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai akiongea na waandishi wa habari.


Mbunge wa Ilala Mh. Zungu akijibu maswali.


Mbunge wa Bariadi Mashariki Mh. John Cheyo akijibu maswali kwa waandishi wa habari.


Mbunge wa Viti Maalum ambae pia ni Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Utawala Mh. Angellah Kairuki akijibu swali toka Kwa Baraka Baraka.


Picha ya pamoja Baada ya Mkutano na waandishi wa habari.

Wabunge wanne waliokuja Uingereza kuzungumzia mgogoro wa pesa za kampuni inayouza vifaa vya ulinzi –BAE Systems wamefafanua namna zitakavyotumiwa. Wakiongea katika Ubalozi wetu Uingereza mjini London, Ijumaa mchana, viongozi hao walihimiza wanachofanya ni kufuatilia matokeo ya mahakama ya sheria inayochunguza rushwa (Serious Fraud Office-SFO) maana kadri muda unavyokwenda ndivyo riba inaongezeka.

Wabunge walikutana na House of Lords ambao ni maofisa na viongozi wa ngazi za juu sana wenye usemi mzito katika masuala ya kisiasa Uingereza.

Mwezi Desemba mwaka jana SFO iliiamuru kampuni ya BAE kulipa faini paundi laki tano na kuipa serikali ya Tanzania paundi 29.5 milioni sawa na shilingi 75.3 bilioni za kitanzania kama pesa za kujisafisha uso. Toka tamko hilo litokee miezi sita iliyopita imezuka migogoro kadhaa.

Upande mmoja BAE system wanataka fedha zisipewe serikali ya Tanzania bali kwa mashirika ya fadhila toka nchi za nje upande mwingine uongozi wa Tanzania unasisitiza serikali inao mfumo imara utakaohakikisha fedha zitawafikia wahusika.

Mgogoro ulianza mwaka 1999 wakati Tanzania ilipotaka kununua vifaa vya kusaidia ulinzi wa viwanja vya ndege toka kampuni ya BAE. Ilidaiwa kuwa mfanya biashara Shailesh Vithlani wa kampuni ya Merlin aliyefanya dili kati ya BAE na Tanzania alipewa asilimia 30 ya pesa ya mauzo kama hongo. Pesa hizo ziliwekwa katika akaunti yake ya benki Uswisi. Wahusika wengine ni aliyekuwa Wakili wa Serikali, Andrew Chenge na Gavana wa benki kuu, Idriss Rashid. Wote hawajashtakiwa na Vithlani anadaiwa kujificha Uswisi, ilhali SFO imetoa tamko afikishwe mahakamani.

Akijibu swali kuhusu kutokuelewana huku, mwenyekiti wa msafara Mbunge Job Ndugai ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, alisema si vizuri BAE kutuingilia au kutueleza nini cha kufanya na pesa hizo ambazo ni maslahi yetu .

“Sisi tunafahamu mfumo gani utakaohakikisha pesa hizo zinatumika sawasawa, zikienda kwa mashirika ya ufadhili ni kama zimetolewa kwa watu wa nje.”

Mbunge mwingine, John Momose Cheyo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge inayohusika na Hesabu za Umma, aliwahakikishia wanahabari kwamba katika miaka kumi toka tukio hilo la 1999 vyombo vya serikali dhidi ya rushwa vimebadilika na kuimarika. “Matumizi halali ya fedha yatakahakikisha pesa zitatumika kujenga elimu,” alisema Mbuge huyo wa Bariadi Mashariki.

Toka SFO ilipoamuru BAE Systems ilipe faini kwa mahakama na fidia kwa Tanzania yametokea pia madai kwamba wapo walioandikia BAE barua pepe kuwa wasiilipe serikali ya Tanzania pesa hizo.

Wabunge wanasisitiza pesa zitaendeleza elimu.


Mbunge Maalum, Angellah Kairuki ambaye ni pia Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki na Utawala, alielezea kwamba ingawa pesa hizo zinaonekana nyingi lakini hazitasuluhisha matatizo yote ya elimu nchini, mathalan, kuongeza mishahara ya waalimu.

Alitoa mifano ya ukosefu wa madaftari, vyoo na vitabu vya kusaidia waalimu kufundisha. Mifano hiyo inayolenga shule za msingi na sekondari inatokana na matizo makubwa ya wanafunzi kujisaidia porini na kukosa vifaa muhimu vya elimu.

Mbunge Mussa Zungu wa Ilala, na vile vile Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje, alikumbusha kwamba tatizo halikuanzwa na Watanzania. “Ni suala lililoamuliwa na mahakama ya Uingereza; sisi tuchohitaji ni kuendeleza elimu.”

Habari imeandikiwa na Freddy Macha akishirikiana Jestina George pamoja na

URBAN PULSE CREATIVE.

MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANZANIA.
Habari kwa hisani ya MO-BLOG

No comments: