Mwenyekiti wa Kanda ya Mbeya wa Tamongsco, Mzee Asanga akitoa utambulisho katika mkutano huo. |
Wamiliki
wa Shule na Vyuo, Wakuu wa Shule na Mameneja wakiwa kwenye mkutano mkuu wa
Mwaka wa Tamongsco Kanda ya Mbeya.
|
CHAMA
cha wamiliki wa vyuo na shule zisizokuwa za Serikali(TAMONGSCO) Kanda ya Mbeya
kimeitaka Serikali kupandisha wastani wa ufaulu wa wanafunzi wakati wa kuvuka
kidato kimoja kwenda kingine kutoka 30 ya sasa hadi 50.
Wito
huo ulitolewa na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa TAMONGSCO Taifa, Mringe
Mzava, katika mkutano mkuu wa kawaida waKanda ya Mbeya uliofanyika katika
ukumbi wa Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino(SAUT) kilichopo Mwanjelwa jijini
Mbeya.
Mzava
alisema kiwango kilichowekwa na Serikali cha kuwabana wanafunzi kuvuka kidato
ni kidogo sana kiasi kwamba kinapunguza morali ya wanafunzi kujisomea hali
inayopelekea kuwa na viwango vidogo vya elimu na kupungua kwa wastani wa ufaulu
katika matokeo ya kidato cha nne.
Alisema
shule zisizokuwa za serikali zimeweka wastani mkubwa jambo linalochangia
shule hizo kufaulisha zaidi kuliko shule za serikali ambapo aliishauri Serikali
kupandisha wastani huo kutoka 30 hadi 50 ili shule zote ziwe na wastani mmoja
na kuongeza ufaulu kitaifa.
Alisema
kwa hali ilivyo si rahisi sana kuendelea kupata wataalam watakaweza kulisaidia
taifa katika maswala ya maendeleo kutokana na wengi kutokuwa na matokeo mazuri
ambapo asilimia kubwa wanatengenezewa matokeo kutokana na Wanasiasa kuingilia
mfumo wa elimu.
Aidha
alitoa wito kwa Wamiliki wa Shule wengine kuacha kupokea ada kwa wanafunzi
ambao hawajakidhi vigezo vya kujiunga na shule ama kuendelea na kidato kingine
bila kuwarudishia jambo alililodai ni kuhujumu uchumi wa wazazi na kupelekea
shule zote kuwa na sifa mbaya.
Naye
Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule zisizokuwa za Serikali, Fidelis Mwampoma, alisema
hata kwenye vikao vya wakuu wa Shule walikubaliana kuishauri Serikali ili
ipandishe wastani huo kwa kuwa ni mdogo na unapunguza ari ya kujisomea
wanafunzi.
Alisema
Wanafunzi wengi wanaosoma kwenye shule za Serikali wamebweteka na
hawajishughulishi kutokana na kuwekewa kiwango kidogo cha ufaulu, hivyo Serikali
inapaswa kuangalia upya kiwango hicho kwa maslahi ya taifa ili kuwe na wasomi
wengi na wenye kujituma.
“
Sisi Wakuu wa Shule hatujakubaliana na wastani uliowekwa na Serikali kwani ni
mdogo mno na unasababisha wanafunzi wabweteke, hivyo ni bora wastani ukapanda
kutoka 30 hadi kufikia 50 hii itasaidia kuongeza nguvu ya kujisomea” alisema
Mwampoma.
Alisema
Serikali isipoliangalia kwa ukaribu suala hilo kuna uwezekano wa kupata
wataalamu wasiokidhi vigezo na wasiokuwa na uwezo kabisa wa kufanya mambo ya
maendeleo na badala yake watapatikana watu ambao wataendeleza ubabaishaji
utakaoligharimu taifa.
“Mambo
mengine Serikali inapaswa kuiga kutoka kwenye Shule zetu mbona na sisi kuna
vitu tunaiga kutoka kwao, Serikali inachojaribu kufanya ni sawa na timu za
mpira wa miguu zinapocheza uwanjani lakini zikashindwa kufungana ukaamua
kupanua goli utakuwa huzisaidii timu” alisema Mwampoma.
Na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment