WADAU wa Mahakama wametakiwa
kuzingatia weledi na maadili ya kazi zao ili kutokuwa kikwazo kwa raia
kupata fursa ya kuifikia haki yao.
Wito huo ulitolewa na Mwakilishi wa Mwanasheria
wa Serikali mfawidhi Kanda ya Mbeya, Archiles Mulisa alipokuwa akitoa mada
kuhusu siku ya sheria katika maadhimisho ya kuashiria kuanza kwa
mwaka mpya wa shughuli za Mahakama ya Tanzania, maarufu
kama siku ya sheria ( law day) yaliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama
kuu kanda ya Mbeya.
Mulisa alisema Fursa ya kupata haki ipo
katika mashauri ya jinai na yale ya madai hivyo ili kuwa na fursa ya
kupata haki ni lazima mamlaka za serikali, mahakama na wadau watimize wajibu
wake ipasavyo na kuongeza kuwa pasipo kufanya hivyo haki haitapatikana kwa
wananchi na hivyo kujenga jamii yenye manung’uniko dhidi ya serikali.
Alisema ni Wajibu wa serikali kuhakikisha
kuwa taasisi zake zinazojihusisha na utoaji wa haki zinatekeleza majukumu yake
kwa weledi na kwa misingi ya haki ili raia wake wawe na fursa ya kupata
wanayostahili kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa Mahakama ambayo ndicho
chombo cha mwisho katika kutafsiri sheria na kutoa haki kina wajibu mkubwa pia
wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fursa ya kupata haki.
“ Kimsingi katika kutoa fursa kwa raia kupata haki
Mahakama ina wajibu wa kutumia sheria zilizopo na kufanya tafsiri yake kwa
ufasaha. Hali halisi sheria haziwezi kutaja kila kitu kinachoweza kutokea hivyo
ni Mahakama zinazoamua kwa njia ya kulinganisha kesi, sheria na maamuzi ya
mahakama yaliyotangulia” alisema Mwanasheria huyo.
Naye Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo
ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Mbeya, Jaji Noel Chocha,
alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuashiria kuanza kwa mwaka mpya wa
shughuli za mahakama nchini.
Alisema maadhimisho hayo hubebwa na
kaulimbiu ambayo husema “fursa ya kupata haki wajibu wa serikali, mahakama na
wadau” ambapo alisema sambamba na hilo huendesha maombi maalumu kutoka kwa
viongozi wa dini ili shughuli zitakazofanyika ziwe kwa matakwa ya Mwenyezi
Mungu.
Aliongeza kuwa mwaka 2015 ni mwaka wenye
matukio mengi na makubwa yanayolikabili taifa hivyo Mahakama inatambua kuwa
uwezo wa kuyafikia hayo haiwezekani kwa utashi wa kibinadamu isipokuwa kwa
uwezo wa Mwenezi Mungu kupitia maombi ya viongozi wa dini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Abbas Kandoro, ambaye alikuwa Mgeni wa heshima katika salamu zake, alisema
Wananchi wanapaswa kutambua kuwa haki inayotakiwa kutolewa kwa wananchi ina
gharama zake ambazo wahusika wanazichangia.
Alisema gharama ambazo mwananchi anapaswa
kuchangia ili haki zake ziweze kupatikana ni kutii sheria jambo ambalo
litasaidia kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani na kuipunguzia serikali mzigo
wa kufuatilia mambo ambayo hayakupaswa kufanyika endapo utii wa sheria
ungezingatiwa.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment