VIONGOZI wa madhehebu ya dini ya kikristu mkoani
Mbeya wamemtaka Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu
Nchemba,kutokata tamaa ya kugombea Urais katika uchaguzi ujao.
Akisoma tamko kwa niaba ya viongozi wa dini Mkoa
wa Mbeya, Mchungaji Gasto Mwaihuti,katika mkutano wao na waandishi wa habari
uliofanyika katika Hoteli ya Suluti iliyopo Uyole jijini Mbeya, alisema
viongozi wa Dini wanaunga mkono nchi kuongozwa na Vijana.
Mwaihuti alisema Viongozi wa kiroho kutoka Mkoa
wa Mbeya ina unga mkono utafiti uliofanywa hivi karibuni na Asasi ya utafiti wa
kielimu Tanzania (TEDRO) na kutoa majibu kuwa vijana ndiyo wenye uwezo wa
kuongoza Nchi katika uchaguzi ujao na kukubalika zaidi katika jamii.
Alisema Viongozi wa dini wanamuunga mkono
Mwigulu Nchemba kugombea urais katika uchaguzi ujao kutokana na maneno yake,
utendaji kazi na historia yake ya kukemea hadharani Rushwa na ubadhirifu wa
fedha za umma sambamba na matumizi mabaya ya madaraka jambo linaloashiria kuwa
ni kiongozi anayefaa kuliongoza taifa.
“Tunamtaka Mwigului Nchemba kutokata tamaa ya
kugombea uraisi kwa sababu tunajua wazi kuwa kwa kauli yake alisimamia kidete
kukemea kwa uwazi sakata la Escrow lililosababisha upotevu mkubwa wa fedha za
wananchi na kupelekea wananchi kukosa imani na serikali yao” alifafanua
Mchungaji huyo.
Alisema viongozi wa dini wanalazimika kufikia
hatua hiyo kutokana na historia mbalimbali kuonesha jinsi vijana wenye umri
mdogo wanavyoweza kufanya matendo makubwa akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere
ambaye aliweza kusimamia mabadiliko makubwa katika kupigania taifa, upatikanaji
wa uhuru wa Tanzania na mataifa mengine barani Afrika akiwa na umri mdogo.
Aliongeza kuwa hata katika maandiko matakatifu
ya Biblia yanaonesha jinsi wadogo wanavyoweza kuwatawala wakubwa ambapo kwa
umri alionao Mwigulu Nchemba kuwa ni mdogo lakini kwa kufuata maandiko hayo
anaweza kuliongoza taifa hili endapo ataungwa mkono na wananchi kwa ujumla na
kuthamini mchango wake katika kipindi hiki kifupi alichoongoza Wizara ya Fedha
kama Naibu Waziri.
“ Maandiko matakatifu ya Biblia yanatuambia kuwa
mdogo atamuongoza mkubwa kwa mfano Yakobo na Esau ambapo Yakobo alichukua
nafasi ya Essau ambaye alikuwa Mkubwa, Mfalme Daudi ambaye alikuwa kijana mdogo
shujaa, hodari na aliyekuwa amesahaulika katika watoto wa Yese ndiye
aliyechukua nafasi ya ufalme licha ya udogo wake hivyo hata sisi viongozi wa
kiroho Mbeya tunaona Mwigulu anafaa” alisisitiza Mchungaji Mwaihuti.
Sambamba na hilo Viongozi hao wa kiroho mkoani
Mbeya waliwataka wananchi wote kuendelea kuliombea Taifa katika kipindi hiki
cha kuelekea katika uchaguzi mkuu ili uwe wa amani na hatimaye kuwapata
viongozi wenye hofu ya Mungu, asiyekuwa na ubaguzi wa kidini, kabila na zaidi
wenye uwezo wa kuwaunganisha watu wote.
Aidha waliongeza kuwa Taifa la Tanzania
linahitaji Kiongozi msafi asiyekuwa na chembe ya mashaka machoni mwa Watanzania
ambaye atakuwa anachukia rushwa na kuikemea hadharani bila kuwaogopa hata
marafiki zake.
“ Ni ukweli usiofichika kuwa taifa letu linapita
katika majaribu makubwa mfano migogoro ya kidini, kukithiri kwa rushwa katika
sekta mbali mbali na maeneo muhimu ya huduma za jamii, mmonyoo wa maadili kwa
viongozi pamoja na kushuka kwa kiwango cha elimu hivyo tunawaomba watanzania
wote kuomba kwa pamoja ili yote hayo yamalizwe kupitia uchaguzi ujao” walisema
viongozi hao.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment