Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Alhaji Mwangi Kundya, akiwahutubia wananchi wa Jiji la Mbeya katika sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa CCM katika viwanja vya RuandaNzovwe. |
Waendesha pikipiki wakiwa katika
maandamano wakiingia katika uwanja wa shule ya Msingi Ruandanzovwe.
|
Meza kuu wakifuatilia kwa makini
mambo yanayoendelea katika uwanja wa Shule ya Msingi Ruandanzovwe.
|
. Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya
mjini, Kulwa Mironge, akiwatambulisha wageni mbali mbali waliohudhuria sherehe
za miaka 38 ya kuzaliwa CCM.
|
Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi
(CCM) Mbeya mjini, Philemon Mng'ong'o akimkaribisha Awilo kutoa burudani kwa
wageni mbali mbali.
|
. Awilo akitoa burudani sambamba na mtoto wake. |
Bendi ya Baby TOT ikiendelea kuwaburudisha wakazi wa Jiji la Mbeya. |
Kikundi cha burudani cha Makhiri khiri kikitoa burudani. |
. Ngoma ya asili ya Kinyakyusa
maarufu kwa jina la Ling'oma kutoka Airport jijini Mbeya ikitumbuiza uwanjani.
|
Wananchi wakifuatilia kwa makini
hotuba za viongozi.
|
CHAMA
cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya mjini kimeadhimisha miaka 38 tangu
kuzaliwa kwa chama hicho kwa kuwakumbusha wananchi kujiandikisha katika daftari
la kupigia kura.
Mjumbe
wa Mkutano mkuu taifa kupitia Wilaya ya Mbeya mjini(MNEC) Sambwee Shitambala,
alitoa wito huo katika sherehe zilizofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi
Ruandanzovwe jijini Mbeya.
Shitambala
alitumia nafasi hiyo kuwasihi Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
kwenye daftari la kudumu la kupigia kura na kuhakikisha wanapata vitambulisho
vitakavyosaidia wakati wa uchaguzi mkuu pamoja na kuipigia kura Katiba mpya.
Alisema
vitambulisho vya sasa ni vizuri kutokana na kuwa vya kielektroniki ambavyo
vitasaidia kuwadhibiti watu wasiowaaminifu ambao huwa na utaratibu wa kupiga
kura mara mbili mbili kwa kuhamishwa eneo moja kwenda lingine.
Aidha
Shitambala alitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kupiga kura za potelea
mbali kwa lengo la kuwakomesha baadhi ya wagombea kutokana na kuenguliwa kwenye
kura za maoni kwamba tabia hiyo inaligharimu taifa kwani baadhi ya
wanaochaguliwa wanakuwa hawana sifa ya kuongoza.
Alisema
katika tathimini ya Viongozi waliochaguliwa katika Serikali za mitaa wengi wao
ni miujiza tu kwani hawana uwezo wa kuongoza na hata kuelewa maana ya kuwa
kiongozi hawaijui kutokana na kuchaguliwa kiholela baada ya wananchi kuchagua
kwa kumkomesha mtu ama Chama.
Kwa
upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Alhaji Mwangi Kundya ambaye alikuwa
mgeni rasmi katika sherehe hizo, aliwashukuru Wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa
kuipa CCM ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika
Disemba 14, mwaka jana.
Kundya
alisema kwa mtu mwenye akili timamu na katika mfumo wa vyama vingi vilivyoamua
kuunganisha nguvu ili kushindana na Chama tawala lakini kimeshindwa kufikisha
hata asilimia 20 ya kura zote ni wajibu kuwashukuru wananchi kwa kuendelea
kuonesha imani kubwa kwa CCM.
Alisema
vyama vingi vilianzishwa miaka 23 iliyopita lakini tangu hapo hawakuwahi kupata
kiongozi yoyote hata ushindi mdogo katika chaguzi zilizopita ndiyo maana baada
ya kuambulia viti hivyo vichache wakaona ni vema kukodi magari na kuanza
kushangilia mitaani.
Katibu
huyo aliongeza kuwa katika uchaguzi uliopita kwa Mkoa wa Mbeya CCM ilipata
ushindi mkubwa tofauti na ilivyokuwa inatarajiwa kutokana na kuwepo kwa wabunge
na madiwani wa Vyama vya upinzani kuwa wangesababisha kushindwa kupata matokeo
mazuri.
Alisema
Mkoa wa Mbeya wenye Vijiji 841 CCM imeshinda ngazi ya Uenyekiti katika vijiji
699 sawa na asilimia 83.12 huku vyama vyote vya upinzani vikigawana asilimia
16.88, kati ya Wajumbe 9195 CCM imepata wajumbe 7295 sawa na asilimia 83.62 na
wapinzani wakipata wajumbe kwa asilimia 16.38.
Kundya
aliongeza kuwa katika ngazi ya Wajumbe wa viti maalumu kwa Mkoa wa Mbeya
walikuwa wagombea 5990 lakini CCM imepata wajumbe 5009 sawa na asilimia 83.62
na kuwaacha wapinzani wakiambulia asilimia 16.38, na kati ya Vitongoji 4445 CCM
imepata vitongoji 3588 sawa na asilimia 80.72 na wapinzani wakiambulia asilimia
19.28 kati ya kura zote.
Katibu
huyo aliongeza kuwa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya lenye mitaa 181 CCM
ilipata Mitaa 107 sawa na asilimia 59.12 na vyama vya upinzani vikiambulia
asilimia 40.88 na hii ni kutokana na kuwa na Mbunge pamoja na madiwani katika
baadhi ya Kata.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
1 comment:
Kweli sherehe hii Mbeya haikuvutia kabisa. Uwanja wenyewe majani marefu inaonekana maandalizi hayakufanyika vya kutosha kama ilivyokuwa Songea. Uwanja huo kama ni muhimu kwa matukio maalum kwa nini haufanyiwi ukarabati ukawa katika hadhi nzuri. Yaani uko shaghalabaghala tu da! ndo CCm hiyo jamani
Post a Comment