WENYEVITI
wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya wameiomba Serikali
kuwaongezea kiwango cha posho ili kiendane na maafisa Watendaji.
Aidha
wametoa ombi la wao kutaka kulipwa mishahara kutokana na kuwa wawakilishi wa
wananchi na sio kupewa posho jambo ambalo linasababisha wao kudharaulika na
watendaji wa Mitaa yao.
Hayo
yalitolewa na Wenyeviti wa Mitaa wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya
walipokuwa wakizungumza na Kaimu Mwanasheria wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya,
Crispin Kaijage, kabla ya zoezi la kuwaapisha lililofanyika katika ukumbi wa
Shule ya Sekondari ya Mbeya.
Braiton
Dibinze Mwenyekiti wa Mtaa wa Kati Kata ya Ruanda alisema kwa mujibu wa Katiba
ya nchi sura ya 4 ibara ya 1 hadi ya 3 ya uchaguzi wa serikali za Mitaa,
Mwenyekiti wa Mtaa ana ainishwa kama mtawala na mwakilishi wa Raisi katika
ngazi ya Mtaa lakini hapewi mshahara kama Watendaji wanaoteuliwa na Mkurugenzi
wa Halmashauri.
Alisema
kitendo hicho sio kizuri kwa kuwa wao ndiyo wenye majukumu ya kuhamasisha
wananchi kuhusu shughuli za maendeleo hivyo walipaswa kupewa kipaumbele cha
malipo tofauti na ilivyo sasa.
“
mimi Mwenyekiti wa Mtaa natambulika kikatiba kama mwakilishi wa Raisi katika
ngazi za Mtaa lakini mtu ambaye ajira yake inaishia kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri analipwa vizuri tunaomba Serikali ilifikirie hilo” alisema Mjumbe
huyo.
Kwa
upande wake Kaimu Mwanaasheria wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Crispin
Kaijage, alisema Mwenyekiti wa Mtaa anapewa Posho ya kila mwezi inayotambuliwa
kisheria ambayo ni shilingi 20,000 kwa mwezi sawa na Madiwani ambao pia hupewa
posho na sio mshahara.
Aliongeza
kuwa kazi ya Mwenyekiti wa Mtaa ni kumsaidia Afisa Mtendaji wa Kata kwa
kumsimamia na kumshauri Afisa Mtendaji wa Mtaa kuhusu shughuli za maendeleo
pamoja na uwajibikaji wake ili kuondoa ulegevu na kuchelewa maofisini.
“
Ofisi wa Mtaa iko chini ya Afisa mtendaji wa Kata, hivyo tuwe walezi wa Maafisa
Watendaji wa Mitaa pamoja na kuwabana ili wafike maofisini kwa wakati na
kutoa taarifa kwa yule anayekiuka utaratibu wa kutekeleza majukumu yake ya kila
siku.” Alisisitiza Mwanasheria huyo.
Alisema
kitendo cha kuwaapisha viongozi hao kinawapelekea kufanya kazi za serikali
katika ngazi za Mitaa wakishirikiana na Maafisa Watendaji kwa mujibu wa sheria
na sio kufanya shughuli za kichama.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment