WAKULIMA
wa Mpunga Wilayani Mbarali wametakiwa kujiunga na vikundi ili
wawezeshwe na kupewa elimu ya uzalishaji wa mpunga kupitia mashamba darasa.
Imeelezwa
kuwa pia Halmashauri hiyo imejipanga kuimarisha mashamba darasa kwa ajili
ya kufundishia wakulima wa kilimo cha mpunga ili kuongeza uzalishaji.
Hayo
yalibainishwa na Afisa Kilimo Mazao wa Wilaya ya Mbarali, Geophrey
Mwamengo, wakati wa zoezi la kupandikiza Mpunga katika shamba darasa lililopo
kwenye Skimu ya Umwagiliaji ya Ipatagwa wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya.
Mwamengo
alisema Halmashauri imebaini ongezeko la uzalishaji wa Mkulima mmoja mmoja
baada ya kutoka na teknolojia sahihi katika mashamba darasa hali
iliyopelekea kuongeza nguvu katika kuboresha mashamba darasa katika Wilaya
hiyo.
Alisema
uzalishaji wa mpunga katika mashamba ya kawaida kwa Wilaya ya Mbarali msimu wa
mwaka 2013/2014 ilikuwa ni wastani wa Tani 4.5 kwa hekta ili hali
uzalishaji wa vikundi katika Mashamba darasa yalikuwa Tani 10 kwa Hekta na
kuongeza kuwa hadi sasa kuna mashamba darasa 19.
Aliongeza
kuwa baadhi ya wakulima wakitoka kwenye mashamba darasa na kila mtu kujilimia
Shamba lake mavuno huongezeka mara mbili zaidi ambapo katika msimu wa mwaka
2013/2014 pato la mkulima binafsi lilikuwa ni Tani 15 kwa Hekta.
Afisa
huyo alisema kutokana na hali Halmashauri imejipanga kuimarisha miundombinu ya
umwagiliaji, ushirika na umoja wa wakulima wanaotumia maji na kuboresha
matumizi ya zana bora za kilimo.
Kwa
upande wake Bwana Shamba wa Kata ya Mahongole, Fredy Amir, alisema matokeo ya
mashamba darasa ni mazuri kutokana na hali za wakulima kubadilika kiuchumi
ambapo asilimia kubwa wanamiliki vyombo vya usafiri pamoja na kujenga nyumba
nzuri.
Alisema
hivi sasa wamejikita zaidi katika kuwahamasisha Wakulima kuendesha kilimo
Shadidi kutokana na kilimo hicho kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo
husababisha mvua kuwa chache hivyo kutoa hofu kwa wakulima.
Alisema
kilimo hicho hakitumii maji mengi hivyo huchangia kupunguza migogoro ya maji
katika jamii kwa ujumla kwa kuwa aina hiyo ya kilimo huhitaji maji machache
ambapo baada ya wakulima kupewa elimu husaidiana kupunguziana maji mashambani.
Naye
Bwana Shamba kutoka Ofisi za Umwagiliaji Kanda ya Mbeya(PHRD), Talibo, ambao
ndiyo wafadhili wa Mashamba darasa hayo alisema kama Ofisi husaidia
kuwahamasisha wakulima kili,mo Shadidi kutokana na kutumia maji machache.
Alisema
Ofisi ya umwagiliaji huvisaidia vikundi kupitia mashamba darasa kwa kuwapatia
mahitaji yote muhimu yanayohitajika wakati wa kuandaa shamba hadi mavuno ambapo
baada ya kuvuna mazao hubaki kwenye kikundi.
Aliyataja
baadhi ya mahitaji kuwa ni pamoja na mbegu za kupanda, mbolea za kupandia,
mbolea za kukuzua, dawa za kuulia wadudu na mashine za kutumia wakati wa
palizi.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
1 comment:
Ni vema sana kwa wakulima kupata elimu ya upandaji mpunga. Lakini afya ni ya muhimu. Angalia akina mama hao hawana boots kiasi kwamba wataathiri afya zao jamani. Watoe na elimu ya afya ya kujikinga na vijidudu miguuni na mikononi wanapofanya kazi sehemu zenye maji kama hapo.
Post a Comment