picha na Mbeya yetu.
UKARABATI wa Barabara ya Lami
iliyochimbika inayotoka Iganzo kuelekea Kabwe jijini Mbeya umezua maswali mengi
kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na hatua zinazofanywa.
Baadhi ya Wakazi hao wamelalamikia kitendo cha Halmashauri ya
Jiji la Mbeya kukarabati barabara hiyo iliyochoka lami yake kwa kujaza vifusi
vya mawe juu yake pasipo kutindua ile ya awali.
Ukarabati wa barabara hiyo
yenye urefu wa zaidi ya Kilomita moja ulianza jana majira ya asubuhi ambapo
Mkandarasi wa barabara hiyo hakujulikana mara moja licha ya magari na mitambo
ya Mkandarasi wa Kampuni ya CCCC inayojenga barabara ya Mbeya – Lwanjiro kutumika
katika ujenzi huo.
Kwa mujibu wa wakazi hao
walisema kitendo cha Halmashauri ya Jiji kumwaga vifusi juu ya lami iliyochoka
ni kufuja fedha za walipa kodi kutokana na vifusi hivyo kuwa na uwezekano wa
kusombwa na maji katika kipindi hiki ambacho Mkoa wa Mbeya unamvua kubwa.
Wakazi hao waliongeza kuwa kawaida
kunakuwa na vibao vinavyoonesha Mkandarasi wa barabara pamoja na Mkandarasi
mshauri lakini vitu hivyo havijawekwa huku ikionekana magari maitambo ya
wachina kukodiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya likilazimika kujaza mafuta
katika mitambo hiyo.
Hata hivyo mmoja wa Mafundi wa
Kampuni ya CCCC ambaye hakutaka jina lake kuandikwa alisema ukarabati wa
barabara kwa muda mfupi kuna hatua ambazo zinapaswa kufuatwa wakati ujenzi
mkubwa unasubiriwa ili barabara iweze kudumu kwa kipindi Fulani.
Fundi huyo alizitaja hatua hizo
kuwa ni kutindua lami ya awali kasha kumwaga udongo wa chini(Sir base) kasha anafuata
kumwaga kokoto(stone base) kasha anamalizia na Lami laini ambayo inaweza kudumu
kwa miaka mitano wakati uongozi ukijipanga kutafuta fedha za kufumua barabara
na kuijenga upya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Jiji la Mbeya, Musa Zungiza, alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuwafafanulia
wananchi juu ya malalamiko hayo lakini simu yake iliita kwa muda mrefu bila
kupokelewa jambo lililolazimu kutafutwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya miundombinu
ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Sheikh Dormohamed Issa.
Mwenyekiti huyo alisema hana
taarifa kuhusu kuanza kwa ukarabati barabarani jambo alilosema kilichokuwa
kikisubiriwa ni upatikanaji wa fedha na kuahidi kulifanyia kazi kwa kumtafuta
Injinia wa Jiji la Mbeya ili kujiridhisha na hatua hizo.
Sheikh Issa aliongeza kuwa
pamoja na ukarabati kuendelea lakini hakuna watakachokuwa wamekifanya endapo
hawatatindua lami za zamani kwani vifusi hivyo vitaweza kusombwa na maji
kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha
hivi sasa.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
1 comment:
Kwa kweli hata mie nisiyejua ujenzi wa barabara naona hapa wamechemsha kabisa. Utajengaje nyumba bila msingi? huku ni kushindwa kazi kwa wawekezaji wa nje. Mbona hata wawekezaji wa ndani wasingefanya hilo. Lo! aibu sana sana hata kwa nchi majirani wakiona hili Mbeya!!!!!Magufuli kaona hili kweli!!!
Post a Comment