WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa katikati ya sherehe za
maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwake, baadhi ya vijana ambao ni wanachama
wa Umoja wa Vijana (UVCCM) mkoa wa Mbeya wameibuka wakiwa na mabango
kumshinikiza Waziri Mkuu mstaafu John Samwel Malecela kuacha kuingilia masuala
ya vijana ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Vijana hao pia wamemtaka Katibu wa Uenezi wa UVCCM, Paulo
Makonda kumwomba radhi Lowassa kwa maneno aliyoyatoa hivi karibuni kwenye
vyombo vya habari kwa madai hawakumtuma afanye hivyo na kauli zake zinalenga
kukigawa chama.
Mjumbe wa Mkutano
Mkuu wa CCM Taifa kupitia UVCCM mkoa wa Mbeya, Rabson Mwaipula alisema kuwa
Malecela ni kiongozi aliyestaafu hapaswi kuingilia masuala ya vijana na badala
yake akae atulie na kula pensheni yake kwa amani.
“Malecela kwa hili amekuwa kama mchezaji ambaye yupo uwanjani
lakini hajui anacheza namba ngapi na hajui anacheza na nani, tunamshauri aache
kucheza mchezo ambao haumfai na badala yake atulie atushauri vizuri, sisi
vijana yale tunayo tenda” alisema Mwaipula.
Alisema kitendo cha Malecela kuanza kuingilia kati masuala ya
vijana na kumshambulia Waziri Mkuu mwenzake mstaafu, Edward Lowassa kinaonyesha
jinsi Malecela asivyotumia vizuri busara zake kukiunganisha chama na badala
yake anakigawa.
Alisema Malecela kama anataka aache posho anazolipwa kama Waziri
Mkuu Mstaafu arejee kwenye ulingo wa Siasa kwani anaonekana bado anautamani
licha ya kuangushwa vibaya kwenye jimbo lake la Mtera mwaka 2010.
Mwanachama mwingine wa UVCCM, Kisumba Mdesa ambaye alikuwa
mwenyekiti wa mkutano wa vijana hao na wandishi wa habari jana jijini Mbeya
alisema Makonda haijui vizuri CCM na historia ya viongozi wa CCM katika mchango
wao wa kukijenga chama, hivyo kitendo chake cha kumshambulia Lowassa kwenye
vyombo vya Habari ni utovu wa nidhamu.
Alisema kuwa Makonda hana sifa ya kuizungumzia UVCCM kwa kuwa
yeye alichaguliwa kuongoza Chipukizi, lakini yeye amejingiza na kujifanya kuwa
ni msemaji wa UVCCM.
Naye David Mwakalinga, ambaye alijitambulisha kuwa ni Mwenyekiti
wa UVCCM kata ya Maendel.eo Jijini Mbeya, alisema Makonda anapaswa kujua
hisitoria za viongozi wa wa juu wa CCM badaya ya kuibuka kwenye vyombo vya
habari na kuropoka.
Alisema kiongozi kama Lowassa, amefanya mambo makubwa hapa
nchini hasa kwa kusimamia maamuzi magumu, pamoja na miradi ya maendeleo kama
shule za kata.
Alisema enzi za uongozi wa Lowassa kama waziri Mkuu alisimamia
kwa nguvu zote ujenzi wa shule za kata ambazo sasa zimeonesha matunda kwa
vijana wa kitanzania kupata elimu katika mazingira safi na kwa gharama nafuu.
Kutokana na hali hiyo wote kwa pamoja waliwaomba radhi viongozi
wa dini, kwani maneno yaliyotewa na wenzao hao ndani ya chama hicho si msimamo
wa wanachama wote.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment