SERIKALI imetakiwa kuondoa mfumo wa
Elimu ya Siasa katika Shule za Msingi na Sekondari na kuingiza somo la Biashara
na kupewa kipaumbele kwa ajili ya Maendeleo katika kukuza uchumi wa mwananchi
mmoja mmoja na Nchi kwa ujumla.
Aidha imeelezwa kuwa somo hilo linapaswa
kupatikana katika ngazi ya chuo kikuu pekee ili kuweka mipaka ya kiutendaji
kuwa na utofauti baina ya Wanasiasa na wataalamu kutoingiza Siasa katika
shughuli za maendeleo zinazosababisha kukwama kwa vitu vingi vinavyosababishwa
na viongozi wa Siasa kuingilia kazi ambazo hawana utalaamu nazo.
Hayo yalibainishwa na Makamu
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mbeya, Graciano Kunzugala wakati akitoa mafunzo kwa
wanachama wa Chama cha Vijana Wanawake Wakristu Tanzania(YWCA) Tawi la Mbeya
yanayofanyika katika ukumbi wa Asasi ya Elimisha uliopo Ilomba Jijini Mbeya.
Kunzugala alisema utaratibu wa
kufundisha Siasa kuanzia ngazi ya chini badala ya biashara umesababisha
viongozi wa Kitaifa kuhubiri zaidi habari ya Umoja Mshikamano na amani bila
kugusia suala la kukua kwa uchumi na fursa za biashara kwa lengo la kukuza
kipato cha nchi na Mtanzania mmoja mmoja.
Alisema hivi sasa Siasa imeingia katika
utendaji hali inayosababisha watu kushindwa kuzungumzia njia mbadala za
kumuinua na kumwezesha mwananchi mwenyekipato cha chini kuongeza kipato chake
ambapo pia amani umoja na mshikamano utapatikana kutokana na kuwa na uchumi
mzuri.
Kwa upande wake Mratibu wa YWCA Mkoa wa
Mbeya, Thabita Bugali, alisema semina hiyo itaendeshwa kwa muda wa siku mbili
ikiwa ni mfululizo wa kuwapatia wanachama mafunzo yatakayoinua asasi ili iweze
kupata mafanikio chanya katika jamii ikiwa ni pamoja na kusaidia kutatua
changamoto mbali mbali zinazoizunguka jamii.
Alisema chama hicho kimepewa mafunzo hayo
kwa ufadhili wa The Faundation for Civil Society,ambapo watapata fursa ya
kujifunza namna ya kuandaa mpango mkakati, uhifadhi wa misitu na vyanzo vya
maji pamoja na Mazingira na usafi wa mazingira kwa ujumla wake.
Naye mwezeshaji katika mafunzo hayo ambaye
ni mwanamazingira na Mwandishi wa Habari, Festo Sikagonamo ambaye pia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Elimisha ambao pia
wamefadhili ukumbi alisema suala la usafi na utunzaji wa mazingira linaanza na
mtu mwenyewe ndani ya kaya yake.
Alisema ili kuondokana na kero ya uchafu
na uharibifu wa mazingira katika jiji la Mbeya ni vema kila Mwananchi akapata
fursa ya kueleweshwa juu ya namna ya utunzaji wa mazingira kwa kuzingatia usafi
pamoja na vyanzo vya maji kwa kutokata miti ovyo.
Alisema endapo Mazingira yakawa masafi
kwa wananchi kuleweshwa kutupa taka katika maeneo yaliyoruhusiwa na kuzolewa
kwa wakati itachangia kuongeza pato la Halmashauri ya Jiji kutokana na Wageni
wengi kuvutiwa na mazingira hali itakayosababisha kukua kwa uwekezaji.
Aliongeza kuwa madhara ya uchafu wa
mazingira na uharibifu wa mazingira ni makubwa sana kwa sababu yanaathiri pia
uchumi wa Nchi na mtu binafsi ambapo kutokana na uchafu wa mazingira mtu
anaweza kupata magonjwa hivyo badala ya kufanya kazi ya uzalishaji atalazimika
kwenda Hospitali kutibiwa magonjwa yatokanayo na uchafu.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment