Picha ya pamoja
MAAFISA Afya na Mifugo wametakiwa
kutobweteka maofisini na kufanyia kazi kwenye makaratasi(Paper Work) badala
yake watumie taaluma yao kama walivyofundishwa mashuleni kwa kufanya kazi ya
vitendo.
Mwito huo umetolewa na Kaimu Mganga Mkuu
wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Agnes Buchwa, alipokuwa akifungua kikao cha
watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Jiji la Mbeya kuhusu Shughuli za Mamlaka
ya Udhibiti wa Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba(TFDA) kilichofanyika leo katika ukumbi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya uliopo Forest Mpya Jijini hapa.
Buchwa alisema kuzagaa kwa uchafu katika
maeneo mengi ya soko na mitaani ni kutokana na kutowajibika kwa maafisa afya na
mifugo ambao ndiyo wenye lengo la kutembelea maeneo mbali mbali ili
kujiridhisha na hali ya usafi wa maeneo na machinjio za mifugo lakini badala
yake wanakaa maofisini na kuishia kuandika kwenye makaratasi.
Alisema hivi sasa TFDA inafanya kazi
ambayo ilitakiwa kufanywa na Halmashauri kwa kuwatumia wataalamu wake ambao ni
Maafisa Kilimo na afya kwa kufunga maeneo yaliyokithiri kwa uchafu ili kuepusha
madhara ambayo yanaweza kuwakumba wananchi kutokana na kutochukuliwa kwa hatua
stahiki.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni
kukumbashana kila mtu wajibu wake ingawa kila mfanyakazi anaelewa lakini
kinachofanyika ni kama matangazo ya biashara yanayojirudia rudia kila mara
yakiwa na lengo la kumkumbusha mnunuaji ndivyo hivyo hata Serikali imeona ni
vema watumishi wake wakapatiwa mafunzo kama hayo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mamlaka
ya udhibiti wa Chakula, Dawa, vipodozi na vifaa tiba(TFDA) Kanda ya Nyanda za
juu Kusini, Rodney Alananga,ambao ndiyo wandaaji wa mafunzo hayo alisema
yamewalenga Maafisa afya, Mifugo, Famasia na wahasibu kutoka Halmashauri za
Wilaya na Jiji la Mbeya.
Alananga alisema wameona ni vema
kukumbushana Sheria za udhibiti wa chakula. Dawa vipodozi na vifaa tiba
kutokana na kujitokeza kwa changamoto nyingi zinazosababishwa na utendaji wa
kazi kila siku ili waweze kujadiliana na kukubailiana namna ya kukabiliana nazo
kwa manufaa ya taifa.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja
na baadhi ya Halmashauri kushindwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika
maeneo mbali mbali hali inayosababisha hatari kwa afya za binadamu ambapo pia
Halmashauri hizo zimeshindwa kuunda Kamati za TFDA na kuzifanyia kazi.
Alisema changamoto nyingine ni pamoja na
Halmashauri kushindwa kutenga bajeti kwa ajili ya shughuli za udhibiti licha ya
kuelezwa katika Sheria na muongozo wa Tamisemi ambapo Halmashauri inapaswa
kutenga Asilimia 40 ya makusanyo yaliyotokana na usajili na shughuli za TFDA na
asilimia 60 kurudishwa makao makuu.
Aliongeza kuwa baadhi ya Halmashauri
ambazo hutenga bajeti hiyo pia zinakabiliwa na changamoto ya kutotumia fedha hizo
kama walivyoelekezwa na badala yake hutumia katika miradi mingine na kuacha
kazi ya udhibiti kutokuwa na fedha hivyo kukwamisha kazi za wataalamu.
Alisema pia taarifa za utendaji kazi za
wataalamu wa Udhibiti haziwasilishwi ofisini jambo ambalo linaashiria kazi hizo
kutofanyika kama inavyotakiwa ambapo mtaalamu anatakiwa kuandaa ripoti kila
anapofanya kazi na kupeleka ofisini ili kuona utendaji kazi wake ikiwa ni
pamoja na Halmashauri kushindwa kupeleka asilimia 60 ya marejesho katika
Mamlaka.
Hata hivyo katika mafunzo hayo wajumbe
walijadili Majukumu ya udhibiti na mipaka ya ufanyaji kazi kati ya Mamlaka na
Halmashauri ambapo Halmashauri zinapaswa kudhibiti utengenezaji, uingizaji,
usambazaji usambazaji wa bidhaa mbali mbali na kukagua maeneo na bidhaa Sokoni.
Na Mbeya yetu
|
2 comments:
Safi sana Dr Agnes buchwa wanawake tunaweza
WAKIWEZESHWA
Post a Comment