JAMII imetakiwa kuelewa kuwa madereva wa pikipiki maarufu
kwa jina la Boda boda ni salama tofauti na wanavyochukuliwa na baadhi ya watu
wakiwaona kama wahuni na wenye kuleta uvunjifu wa amani.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Miradi na utekelezaji wa
Kampuni ya CitySign Promotion &
Marketing Agency Ltd ya Jijini Mbeya, Geophrey Mwangunguru,wakati
akizungumza na madereva wa Pikipiki Jiji la Mbeya kuhusu maandalizi ya kuelekea
kuanza kwa ligi ya Mpira wa Miguu kwa madereva wa Bodaboda katika kikao
kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya City pub.
Mwangunguru alisema lengo la kuandaa ligi kwa ajili ya
madereva wa bodaboda ni kutaka kuifahamisha jamii kuwa nao ni sehemu yao na
siyo waletaji wa vurugu kama wengine wanavyodhani kupitia Mpira wa miguu utakaowakutanisha pamoja na
wanajamii.
Alisema pia lengo la ligi hiyo na matarajio yao ni kuona
Madereva wa boda boda Jiji la Mbeya linakuwa na timu bora na kubwa ambayo
inaweza kushiriki michuano yoyote na wakati wowote ndani na nje ya Mkoa wa
Mbeya ikiwemo Ligi zinazoendeshwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini(TFF).
Aliongeza kuwa Ligi hiyo inatarajia kuanza kutimua vumbi
Aprili 27, Mwaka huu ikishirikisha timu 16 kutoka Kanda 7 za madereva wa Boda
boda na kwamba viwanja vitakavyotumika ni pamoja na Uyole, Iyunga na Mwenge
huku timu zitakazoingia Fainali kukipiga katika uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine.
Aliongeza kuwa suala la zawadi bado linajadiliwa na kamati
ya uendeshaji wa Ligi kutokana na mapendekezo mbali mbali ambapo Mshindi wa
kwanza anaweza kujinyakulia Pikipiki Mpya yenye thamani ya Shilingi Milioni
2.2/=.
Kwa upande wake Mkuu wa Mauzo wa kampuni hiyo, Ibrahimu
Mbembela alisema Kampuni yao kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Jiji
la Mbeya(MUFA) wameandaa Sheria na taratibu mbali mbali za kuendesha ligi hiyo
ambazo wamekubaliana na viongozi wa bodaboda.
Alizitaja sheria hizo na taratibu kuwa ni pamoja na
Usajilii wa wachezaji kuwa 30 ambapo kati yao wachezaji 20 ni madereva wa boda
boda na 10 watatoka nje ya madereva.
Mchezaji haruhusiwi kuchezea timu zaidi ya moja, kikao cha
maandalizi ya mechi husika kitafanyika kila siku asubuhi kabla ya mechi,
mabadiliko ya wachezaji ni watano, mchezo ukivunjika utaendelea pale ulipoishia
kutokana na taratibu husika kufuatwa.
Alizitaja sheria zingine kuwa ni kila timu kuwa na mpira
mmoja ambao watakuwa nao kila mchezo, ada ya ushiriki wa mashindano ni Shilingi
30,000/=, timu ivae jezi yenye namba inayoonekana mgongoni, timu ikichelewa
kufika kwenye kikao cha maandalizi faini 10,000 na timu isipofika kabisa
italipa shilingi 20,000/=.
Aidha aliongeza kuwa taratibu zingine ni kufuata sheria na
kanuni za 17 za mpira wa miguu kama zinavyotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Duniani(FIFA).
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment