Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Tuesday, June 4, 2013

CHUO CHA THE VOICE FROM WILDERNESS MBALIZI BIBLE COLLEGE CHAJITOLEA KUTOA ELIMU BURE KWA WATOTO WA MITAANI, WAFANYA HARAMBEE KUCHANGISHA FEDHA ZA UJENZI WA MADARASA.

Jerry Kabwe (kulia) Mwanachuo wa Chuo cha Biblia Mbalizi ambaye ni raia Congo akimvalisha Beji Mgeni yasmi katika harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa Chuo hicho Yono Stanley Kevela.
Yono Stanley Kevela (kati kati) akiwa amesimama pamoja na viongozi wa dhehebu la pentekosti kabla ya kuanza kwa harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa chuo cha Biblia katika hafla iliyofanyika katika kitongoji cha Mtakuja Kijiji cha Mbalizi Wilaya ya Mbeya.

Mtoto ambaye jina lake halikufahamika maramoja akitoa burudani katika Harambee hiyo.

Mkurugenzi wa Chuo hicho cha The Voice from Wilderness Mbalizi Bible College Mchungaji Alison Kameta akizungumza jambo katika harambee hiyo.


Mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho Mchungaji William Mwamalanga akizungumza jambo wakati wa harambee hiyo.

Mgeni rasmi katika harambee hiyo Yono Stanley Kavela akizungumza na waumini na wananchi waliojitokeza katika harambee hiyo ambapo alichangia zaidi ya shilingi milioni mbili.

Mgeni rasmi Kavela akimkabidhi cheti Mwanachuo anayehitimu masomo ya uchungaji katika ngazi ya Diploma Daniel Mwaigaga.
Baadhi ya waumini na viongozi wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi mara baada ya kukamilika kwa harambee,




ILI kupunguza ongezeko la kasi la watoto wa mitaani, Serikali imeshauriwa kuzisaidia Taasisi zinazojitokeza kukabiliana na tatizo hilo kwa kufungua miradi na kuanzisha shule kwa ajili ya kutoa elimu mbali mbali.


Mwito huo ulitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha The Voice from Wilderness Mbalizi Bible College, Mchungaji William Mwamalanga kilichopo katika Kitongoji cha Mtakuja Mbeya Vijijini Mkoani hapa wakati wa Harambee ya ujenzi wa madarasa ya Chuo hicho kwa ajili ya kitengo cha watoto wa mitaani.



Mwamalanga alisema baada ya kufanya utafiti na kugundua kuwa Watoto wa mitaani wanazidi kuongezeka na kufanya uhalifu kuzidi kushamili ndipo walipoanzisha wazo la kujenga chuo ambacho kitakuwa kikitoa Elimu bure kwa watoto hao kuhusu maisha na ujasiliamali ili kukabiliana na Ujinga miongoni mwao.


Aliongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ndiyo inayoongoza kwa sasa kuwa na watoto wengi wa mitaani ambapo alisema baada ya kutangaza wazo la kutoa elimu bure kwa watoto wa mitaani zaidi ya Watu 900 walijitokeza kuomba nafasi za kuanza kusoma.


“ Kutokana na nchi yetu kukabiliwa na watoto wa mitaani ambao wengi wao huathirika pia na madawa ya kulevya na kugundulika kuwa wengi wao wanaukosefu wa Elimu ndipo tulipoona kuna haja ya kuisaidia serikali kwa kutoa elimu bure katika Chuo chetu lakini Serikali pia inatakiwa kuunga mkono juhudi zetu” alisema Mwamalanga.


Kwa upande wake Mgeni Rasmi katika Harambee hiyo Yono Stanley Kavela,ambaye  pia ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la kutetea haki za Mlaji na Mbunge mstaafu wa Jimbo la Njombe Magharibi kupitia Chama cha Mapinduzi, Mbali na kupongeza jitihada na mawazo ya Mwenyekiti wa Chuo hicho kuhusu mkakati wao wa kupunguza watoto wa mitaani kwa kuwapa elimu bure pia alitoa wito kwa uongozi wa Chuo hicho kuhakikisha wanaotakiwa kusoma hapo wawekewe vigezo maalumu.

Alisema mara nyingi nafasi za bure zinapotokea wanaojazana katika nafasi hizo wanakuwa ni watoto wa wenye uwezo ambo huhodhi nafasi zote na kuwanyima wenye mahitaji halisi ambao pia ndiyo walengwa na kusudio la uanzishwaji wa Chuo hicho.

Alivitaja baadhi ya vigezo vinavyotakiwa kuzingatiwa kwa wanatakiwa kusoma Chuoni hapo kuwa wawe ni watoto wanaotoka katika mazingira magumu, Maskini, Yatima na Wenye vipato vya Chini kabisa ambao ndiyo wanaotakiwa kupewa kipaumbele lakini kwa wenye uwezo wanatakiwa kuchangia ili kuwezesha Chuo kuwa endelevu.


Naye Mkurugenzi wa Chuo hicho Mchungaji Alison Kametaalisema Chuo hicho kilianzishwa Septemba Mwaka 2003  kikiwa na Wanafunzi 18 wa Kozi za Uchungaji katika ngazi ya Diploma wanayosoma kwa miaka mitatu ambapo hadi sasa Chuo kina Wanafunzi 18 ambapo Mwaka wa Kwanza wako 6, Mwaka wa Pili 8 na Mwaka wa Tatu wakiwa na Wanachuo wawili tu.


Aliongeza kuwa Chuo hicho kinakabiliwa na Changamoto mbali mbali zikiwemo za Upungufu wa Majengo kwa ajili ya madarasa ambapo kwa sasa hulazimika kutumia Vyumba vichache kwa awamu na kupokezana ambapo alisema Vyumba vinavyohitajika kwa sasa ni Vyumba 7 kwa ajili ya Madarasa, Ofisi na Ukumbi ili kuweza kufikia lengo la kupongea watoto 400 wa mitaani pamoja na wanachuo.


Alisema zaidi ya Shilingi Milioni 155 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi huo ambapo Juhudi za Chuo zimefanyika kwa kutumia zaidi ya Shilingi Milioni 60 kujenga baadhi ya Vyumba ambavyo vinatumika hadi sasa na kuiomba Serikali na wadau mbali mbali kujitokeza kusaidia kukamilisha ujenzi huo ili kuwakomboa vijana kwa elimu ili wasiathirike na madawa ya kulevya na kujiingiza katika Shughuli za hatari.


Chuo hicho kinachomilikiwa na Makanisa ya Kipentekosti kinatoa kozi 72 katika ngazi ya Diploma bila kujali dini wala Nchi wanayotoka ambapo huduma zitolewazo ni pamoja na Utume, Uinjilisti, Uchungaji, Ualimu, Unabii na Uongozi wa Kikristu ambapo baada ya kuhitimu Wanachuo hao hupewa vyeo kulingana na Dhehebu analotoka.

  
Katika Harambee hiyo zaidi ya Shilingi Milioni 3 zilichangwa kutoka kwa watu mbali mbali huku Mgeni rasmi Yono Kavela akitoa Fedha Taslimu Shilingi Laki Nane kwa ajili ya ununuzi wa mabati na kuahidi Shilingi Milioni Nne kwa ajili ya ukamilishaji wa Ujenzi wa Vyumba vinne.


No comments: