KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Uongozi wa
Serikali ya Kijiji cha Mpolo kata ya Utengule Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya
imegeuza matumizi ya Zahanati ya Kijiji kuwa Ofisi.
Hilo limebainika baada ya Waandishi wa Habari
kutembelea eneo hilo na kukuta majengo ya Zahanati hiyo yakitumika kama Ofisa
ya Mtendaji wa Kijiji, Ofisi ya Mwenyekiti na Ofisi kwa ajili ya Baraza la
Usuluhishi la Kijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Andres Mlongosi,
alipohojiwa kuhusiana na tuhuma za kugeuza matumizi ya Jengo ambalo lilitakiwa
litumike kwa ajili ya Zahanati lakini wao wanalitumia kama ofisi alikiri
kufanya kinyume kwa kile alichodai Serikali ya Kijiji haina ofisi kutokana na
jengo lilikuwa likitumika awali kubomoka.
Aliongeza kuwa wako kwenye mpango wa kujenga
upya ofisi yao ambapo baada ya kukamilika Jengo hilo litaachwa litumike kama
ilivyokuwa imekusudiwa kwa matumizi ya Zahanati ambapo hadi sasa Wananchi
hupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Utengule, Igurusi au Hospitali ya
Misheni ya Chimala sehemu ambazo ni mbali.
Aidha wananchi hao wameendelea kupata adha ya
matibabu hasa Wanawake wajawazito ambao hutumia muda mrefu kusafiri kufuata
matibabu pamoja na Wazee wasiojiweza ambapo hutembea kwa zaidi ya Kilomita 15.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya
Utengule, Benyanga Zuberi amethibitisha uwepo wa hali hiyo na kwamba
Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ndiyo iliyosababisha hali hiyo kutokana
na kutotuma fedha za kumalizia maeneo yaliyobaki kama Choo.
Alisema suala la kuweka Ofisi kwenye majengo ya
Zahanati ni suala la Mpito ambapo baada ya kukamilika kwa ujenzi kwa asilimia
zote Zahanati itaendelea kama kawaida hivyo Wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu
hali hiyo.
Nao Wananchi wa Kijiji hicho walisema
wanasikitishwa na kitendo kilichofanywa na uongozi wa Kijiji cha kugeuza
majengo ya Zahanati kuwa ofisi licha ya kutumia nguvu nyingi kuchangia ujenzi
huo.
Walisema kitendo hicho si cha uungwana na
kinakatisha tamaa wananchi kuendelea kujitolea nguvu na michango katika
kufanikisha ujenzi na shughuli mbalimbali za maendeleo kama wataendelea kugeuza
matumizi tofauti na inavyokuwa imekusudiwa.
Diwani wa kata ya Utengule Juntwa Mwalyaje
alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba Baraza la dharula lililoketi Mei 6,
Mwaka huu lilikutana kujadili mustakabali wa zahanati hiyo ambapo walimwomba
mganga Mkuu wa Wilaya kuandika barua ya maombi ya fedha za kumalizia ujenzi wa
zahanati hiyo ikiwemu ujenzi wa Choo na Nyumba ya Mganga.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarali
Venance Gwaza Mwashala amesema Halamashauri ilishapitisha Shilingi Milioni Tano
kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya Kwanza ambazo zitaingizwa katika akaunti ya
Kijiji wakati wowote kuanzia sasa
Aidha ameutaka uongozi wa kijiji kuongeza nguvu
zao ili waweze kukamilisha mapema ujenzi huo na kuletewa waganga na huduma zote
ili kupunguza adha kwa wananchi ya kufuata matibabu mbali.
Picha na E.Kamanga
|
No comments:
Post a Comment