UFUNGUZI wa Ligi ya Mpira wa Miguu ya Kombe la
Mwakisu nusura uingie doa kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jana mara tu baada ya
mgeni rasmi kutangaza kuyafungua mashindano hayo yanayofanyika katika Viwanja
vya Shule ya Msingi Mbata Jijini Mbeya.
Mvua hiyo ilianza majira ya saa kumi na nusu
jioni ilileta hofu kwa maelfu ya mashabiki waliofurika katika viwanja hivyo
kushuhudia mechi za ufunguzi katika Ligi iliyozinduliwa na Kaimu Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakael Masaki.
Masaki alisema njia kuuu ya Vijana kuondokana na
uhalifu ni pamoja na kushiriki michezo ambayo huwakutanisha pamoja hivyo kukosa
muda wa kufikiri vitendo viovu ambavyo havina maslahi kwa taifa na kuongeza
kuwa Michezo ni afya hivyo ni jukumu la kila kijana kuhakikisha anashiriki
kikamilifu katika Michezo.
Kwa upande wake mdhamini mkuu wa ligi hiyo ya
Mwakisu Cup, Nwaka Mwakisu alisema ndoto yake kubwa katika maisha ni kuona
vijana hawakosi kazi ya kufanya na ndiyo maana kajitolea kuanzisha ligi ambayo
itawafanya vijana wote bila kujali itikadi za kisiasa kuhudhuria ikiwa ni
pamoja na kushabikia na kushiriki.
Mwakisu alizitaja zawadi zitakazotolewa kwa
washindi wa Michuano hiyo yenye timu 24 zilizogawanywa katika makundi manne
kuwa ni Mshindi wa kwanza atajinyakulia kitita cha Fedha taslimu shilingi
Milioni 2,Msindi wa Pili Milioni 1 na Mshindi wa tatu ikiibuka na Shilingi Laki
tano tu.
Aidha pamoja na mvua kubwa kunyesha mchezo wa
ufunguzi uliozikutanisha timu za Airport Rangers Fc na Terminal Fc uliendelea
hivyo hivyo kutokana na uwanja uliotumika kutotunza maji hivyo kutokuwa sababu
ya kuahirisha mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi wa kati Bitebo Manduta.
Katika mchezo huo timu ya Terminal Fc ilifanikiwa
kuibuka na ushindi wa Magoli 2 kwa Moja dhidi ya timu ya Airport Rangers,
hata hivyo timu ya Airport ilibidi ijilaumu yenyewe kutokana na kukosa magoli
mengi katika kipindi cha kwanza baada ya kujipatia goli la kuongoza dakika ya
kumi ya mchezo kupitia kwa mchezaji wake Amoni Sanga.
Timu ya Terminal ilifanikiwa kusawazisha goli
hilo dakika ya 45 kabla ya mapumziko ambapo timu zilienda mapumzikoni zikiwa
sare ya kutoshana nguvu kwa goli moja moja, kipindi cha pili kilianza kwa kasi
huku kila timu zikishambuliana kwa zamu na kuwaweka katika hali ngumu Walinda
milango kufuatia mpira kuteleza mikononi kutokana na mvua kubwa lakini Terminal
walifanikiwa kufunga goli la pili na ushundi dakika ya 40 ya kipindi cha pili
kupitia kwa mchezaji wake Issa Nelson.
Kwa upande wake mratibu wa ligi hiyo David
Mwakalinga alisema ratiba maalumu ya ligi hiyo haijapangwa vizuri kutokana
na baadhi ya timu kusuasua kujiandikisha ambapo alizitaja baadhi ya timu
zilizothibitisha kushiriki michuano hiyo kuwa ni Airport, Terminal, Zaragoza,
Ghana, Temeke, Maji ya Ugoko, Jangwani, Uhindini, Nyota, Black Eagle, Simike,
Inter Forest, Saitama na Majengo.
Picha na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment