MKUU wa Mkoa wa Mbeya Abbasi Kandoro anatarajiwa
kuwa Mgeni rasmi katika Bonanza lililoandaliwa na Kampuni ya Life Time
Entertainment & Marketing Limited ya Mjini hapa, lenye lengo la kuwakusanya
watu wengi kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo ya Mkoa wa Mbeya.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari katika
Mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Living Stone ya Mjini
hapa, Mratibu wa kampuni hiyo, Venance Matinya alisema Bonanza hilo
litahusisha Taasisi za Umma, Mashirika Binafsi, Wanahabari wa Mkoa wa Mbeya na
Wadau mbali mbali wapenda maendeleo ya Mkoa wetu.
Amesema Bonanza hilo litaitwa “Mbeya Kwanza
Super Bonanza” ambalo litakuwa na lengo la kuwakutanisha waandishi
wa habari na wadau mbali mbali ili kuhamasisha uwekezaji wa ndani na vivutio
vya mkoa wa Mbeya na kukemea dhana potofu juu ya vitendo vya upigaji nondo na
ushirikina vinavyosababisha kukwamisha maendeleo ya Mbeya.
“ Bonanza letu litakuwa na Ujumbe unaosema “
pinga vitendo vya ukatili, migogoro ndani ya jamii, epuka uvunjifu wa amani hamasisha
amani na uzalendo katika mkoa wa Mbeya na Tanzania”hivyo ndugu zangu tusaidiane
kuhamasisha uzalendo wetu” alisema.
Ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa
Bonanza hilo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbasi Kandoro amekubali kushiriki na kuwa
mgeni rasmi katika bonanza litakalofanyika siku ya Jumamosi Oktoba
20, mwaka huu katika viwanja vya shule ya msingi Ruanda Nzovwe.
Mratibu huyo amesema katika bonanza hilo
litakaloanza mapema asubuhi litakuwa na michezo mbali mbali kama vile Mpira wa
miguu(wanaume),netboli(wanawake),kuvuta kamba na riadha kukimbiza kuku na
kuvuta kamba.
“Pia katika ratiba yetu tutakuwa na hotuba mbali
mbali ambazo zitatolewa siku hiyo ambazo zikuwa na ujumbe wa kuhamasisha
uwekezaji wa ndani itakayotolewa na uongozi wa kituo cha uwekezaji kanda ya
Nyanda za juu kusini.
Na kuongeza kuwa, hotuba nyingine itatolewa na
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ambaye atakemea uhalifu na kuhamasisha amani na
utulivu, Mwenyekiti wa Mjata ambaye atakemea vitendo vya ushirikina na
kujipatia mali kwa njia za udanganyifu vitendo vinavyosababisha kukosekana kwa
maendeleo katika mkoa wetu” alisema Matinya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo,
Humphrey Masassi ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa makampuni mbali
mbali kujitokeza kutoa udhamini kwenye matukio yanayo hamasisha maendeleo ya
eneo husika na siyo kusubiri watu wan je kuja kufanya biashara ndani ya mkoa wa
Mbeya.
Masassi amesema Mkuu wa Mkoa pia atatoa hotuba
pamoja na kutoa zawadi kwa washiriki wa bonanza hilo wakiwemo wanahabari ambapo
pia muda huo utatumika kwa ajili ya Benki ya damu salama kutoa elimu kwa
washiriki ili waweze kuchangia damu kwa ajili ya wenzetu walionauhitaji
kutokana na ajali nyingi zinazoendelea kutokea maeneo mbali mbali.
Ameongeza kuwa Mbali na Bonanza hilo pia Kampuni
yake Kwa kushirikiana na SAM ENTERTAINMENT imeandaa uzinduzi wa Filamu
inayoitwa KIJAKAZI ambayo itazinduliwa Oktoba 5 Mwaka huu siku ya Ijumaa katika
ukumbi wa Mkapa ulioko Sokomatola Jijini Hapa ambapo uzinduzi huo utasindikizwa
na wasanii kutoka Dar kama vile Senga na Pembe.
|
No comments:
Post a Comment