Na: Mwandishi wetu
ILE ajali ya kutisha iliyoshirikisha magari matatu, likiwemo la Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya CCM, Mkoa wa Mbeya, Dk. Marry Mwanjelwa na kuua watu 11, imesimuliwa mambo ya kutisha, Risasi Jumamosi linashuka nayo.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 2, mwaka huu, Mbalizi, Mbeya Vijijini ambapo magari matatu, likiwemo lori lililosababisha ajali yaligongana na kupinduka kisha kuwaka moto na kuteketea na baadhi ya watu.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na Risasi Jumamosi, hakuna shaka eneo hilo limetawaliwa na majini kwa vile haupiti mwezi bila kutokea ajali ya kutisha.
“Sisi tunasema hapa kuna majini jamani, hapapiti mwezi lazima itokee ajali, serikali ielewe hilo jamani,” alisema Mzee Simon Mwalusale, mkazi wa ene hilo.
Pia yapo maelezo kuwa, mapema siku ya tukio, kulionekana noti za shilingi elfu kumi zikipeperuka eneo hilo na watu waliziokota.
“Kuna jambo lingine la ajabu sana, siku ya tukio, mapema zilionekana noti za elfu kumikumi, watu waliziokota licha ya kwamba hazikujulikana zilikokuwa zikitokea.
“Cha kushangaza, zile noti zilikuwa na damudamu, lakini hilo watu hawakulijali, waliziokota na kuziweka mifukoni mwao,” aliongeza mzee huyo.
Wakati huohuo, umoja wa wachungaji, Mbalizi, wakiongozwa na mchungaji aliyetambulika kwa jina moja la Daudi wanajipanga kufanya maombi eneo hilo ili kama kuna nguvu za giza zinazosababisha ajali mara kwa mara ziondoke.
Oktoba 4, 2012, jijini Dar katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dk. Mwanjelwa ambaye alifikishwa hospitalini hapo kutoka Mbeya kwa matibabu zaidi, alizungumza na mwandishi wetu akiwa katika chumba maalum cha uangalizi.
“Nilikuwa nikishuhudia ile ajali kwani lori lilikuwa nyuma yetu kwa kasi huku likionekana breki ziligoma na ndipo lilipotuvamia na kutugonga.
“Nilisikia kishindo kikubwa kikitokea, nilijua ndiyo mwisho wa uhai wangu hapa duniani, lakini Mungu mkubwa bado niko hai.
“Nawashukuru wasamaria wema na askari waliokuja kutuokoa, ila nimeumia sana niliposikia kuna watu 11 walikufa na wengine kujeruhiwa vibaya.
“Sasa naendelea vizuri tofauti na nilivyoletwa (Jumatano), nawashukuru madaktari na wauguzi kwa jitihada zao,” alisema Dk. Mwanjelwa.
CHANZO: GLOBAL PUBLISHERS INFO
No comments:
Post a Comment