Makamu wa Raisi wa TCCIA Taifa, Julius Kaijage, akiongea na waandishi wa habari
SERIKALI imetakiwa kutunga sheria
itakayosimamia sera ya uwekezaji na uwezeshaji ili iweze kutekelezeka kwa
vitendo pamoja na kutoa adhabu kwa watumishi watakaoonekana kufanya vibaya.
Wito huo ulitolewa jana na Makamu wa
Raisi wa TCCIA Taifa, Julius Kaijage, alipokuwa akichangia mada katika mkutano
wa baraza la biashara la Mkoa wa Mbeya lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano
wa Mkapa uliopo Sokomatola jijini Mbeya.
Kaijage alisema suala la uwezeshaji na
uwekezaji linatakiwa kupewa kipaumbele kwa kutungia sheria ili sera iliyowekwa
na Serikali iweze klutekelezeka kwa vitendo na kutoa adhabu kali kwa
wanaojaribu kukwamisha.
Alisema sekta binafsi ndiyo zinazoibeba
serikali katika dhana ya uwekezaji hivyo ni vema watawala wakaacha kufanya kazi
kimazoea bali wawe na mipango mkakati inayotekelezeka ili kuifanya sekta ya
uwekezaji kuwa hai ikishirikisha sekta binafsi kwa mapana zaidi.
Aidha alizitupia lawama baadhi ya
Halmashauri nchini kuendelea kukwamisha uwekezaji kwa kushindwa kuwa na
utaratibu mzuri wa kuwalipa wazabuni wanaosambaza huduma mbali mbali katika
ofisi zao.
Alisema Halmashauri hazina kumbukumbu za
kutosha za wazabuni wanawadai na waliowalipa hali inayosababisha wengi kukimbia
kutokana na mfumo mbovu unaotumika kutokuwa rafiki kwa mzabuni ambaye amewekeza
katika kufanya kazi na Halmashauri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Abbas Kandoro, ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Mkoa wa
Mbeya, alisema wafanyabiashara ndiyo wanapaswa kufuata taratibu na sheria za
manunuzi na Halmashauri ili kuepuka malumbano yasiyokuwa ya kawaida.
Alisema wafanyabiashara wengi hufanya
biashara na Halmashauri kwa mazoea bila kufuata taratibu na Sheria za manunuzi
ambapo Mkuu wa idara anatoa maagizo ya kusambaziwa bidhaa ili hali mhasibu
hajui wala Mkurugenzi.
“Tunapozungumzia uwekezaji na uwezeshaji
kwenye Halmashauri zetu, wafanyabiashara ndiyo wenye makosa kutokana na
kufahamiana kwake na mkuu wa idara wanakubaliana pasipo kuweka kumbukumbu jambo
linalokuja kuwa gumu wakati wa malipo” alisema Kandoro.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment