KLABU ya Mbeya City Veteran ambayo
inajumuisha wachezaji wa mpira wa miguu wa zamani imetembelea vituo viwili vya
kulelea watoto yatima na kutoa msaada wa vitu mbali mbali.
Katika Ziara hiyo klabu hiyo
iliyofanyika jana ilitembelea vituo viwili vya Child Support Tanzania
kilichopo Block T Soweto jijini Mbeya na kituo cha Nuru Orphans Centre
kilichopo Uyole ambavyo vilipata msaada wa vitu mbali mbali.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Shaban Robert,
alivitaja vitu hivyo kuwa ni pamoja na Sukari, Sabuni za mche, sabuni za unga,
Vyandarua, Mafuta ya kupikia, dawa za meno na juisi vilivyogawiwa kwa vituo
vyote viwili vikiwa na thamani ya shilingi Laki tatu.
Aidha alitoa wito kwa Taasisi, Asasi za
kiserikali na binafsi zimetakiwa kuwa na utamaduni wa kutembelea vituo vya
kulelea watoto yatima ili kujua changamoto wanazokumbana nazo kwa lengo la
kuvisaidia.
Robert alisema suala la kulea watoto
yatima si jukumu la mwenye kituo bali ni kila mtu mwenye utu wema kwa kuwa hao
watoto hawakupenda kuwa yatima ama kuishi kwenye mazingira magumu.
Alisema endapo kila taasisi ama kundi la
watu kama walivyo Mbeya Veteran wakajenga utamaduni wa kutembelea vituo hivyo
ni rahisi kujua changamoto zinazovikabili na kusaidia kuzitatua jambo ambalo
litamrahisishia mmiliki wa kituo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha
Child Support Tanzania, Noela Msuya, ambaye kituo chake kinahudumia watoto
wenye ulemavu mbali mbali alishukuru kupata msaada huo kuwa utasaidia kuendesha
kituo.
Alisema mbali na watoto hao kulelewa
kituoni hapo kwa muda wa mchana na kisha jioni kurejeshwa makwao lakini
hufundishwa masomo ya awali ukiwemo ufundi, uchoraji na sanaa kwa ujumla.
Naye Meneja wa Kituo cha Nuru, Amanda
Fihavango aliwashukuru Mbeya Veteran kwa kuguswa na namna kituo hicho
kinavyojiendesha na kuamua kutoa msaada utakaowasaidia watoto kuendelea kuishi
na kufurahia maisha kama watoto wengine walioko majumbani.
Alisema kituo chake kinalea watoto
wasiokuwa na wazazi kabisa ambao asilimia kubwa huokotwa kwenye majalala au
kutelekezwa na wazazi wao hivyo kituo kinakabiliana na changamoto za kuwalea
kisha kuwapeleka shule umri unapokuwa umekaribia.
Alisema mbali na changamoto hiyo pia Serikali
ambayo ndiyo huwapeleka watoto hao kituoni hapo kupitia Jeshi la Polisi na
Ustawi wa jamii lakini hakuna msaada wowote anaoupata kutoka Serikalini.
Aliongeza kuwa kwa sasa kituo chake
kinakabiliana na ukosefu wa uzio ili kudhibiti wizi wa vifaa vya watoto ambapo
alitoa wito kwa taasisi na asasi mbali mbali kujitolea kuwajengea ukuta huo.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment