Ulinzi mkali uliimarishwa mahakamani hapo
HAKIMU Mkazi wa Mfawidhi wa Mahakama ya
Wilaya ya Mbeya, Michael Mteite amewagiza wakili kuhakikisha anampeleka
mtuhumiwa mahakamani hata kwa machela.
Hakimu Mteite alilazimika kutoa kauli
hiyo wakati akisikiliza kesi inayowakabili Askari wawili wa jeshi la
Polisi na Magereza pamoja na watu watatu ambao ni raia wa kawaida
wanaotuhumiwa kwa ujambazi wa kutumia silaha.
Kauli ya Hakimu ilikuja kufuatia mmoja
kati ya washtakiwa wote watano kushindwa kuhudhuria mahakamani wakati kesi yao
ilipangwa kuendelea na ushahidi baada ya Wakili wa Serikali Archiles
Mulisa kuhoji Mhakamani kuwa Mshtakiwa namba mbili Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa
Iyela Jijini Mbeya hajafika huku upande wa jamhuri ukiwa hauna taarifa.
Kutokana na hoja hiyo ndipo aliposimama
Wakili wa Utetezi ambaye anawasimamia watuhumiwa wote wato, Ladislaus Lwekaza
na kuiambia Mahakama kuwa Mshtakiwa namba mbili ameshindwa kuhudhuria kesi yake
kutokana na kuwa majeruhi yaliyotokana na kupigwa risasi sehemu ya paja hivyo
kumfanya kuwa na maumivu makali anayougulia akiwa gerezani.
Lwekaza alidai kuwa kutokana na mteja
wake huyo kuwa majeruhi aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi hapo
mtuhumiwa huyo hali yake itakapotengemaa na kuongeza kuwa pia hawataweza
kuendelea na kesi kutokana na washtakiwa wote kutopewa hati za mashtaka na
maelezo ya mlalamikaji ili wajiandae na utetezi.
Hata hivyo Wakili wa Serikali Mulisa
alisimama na kumuuliza Wakili wa utetezi kuwa anapaswa kuiambia mahakama
kifungu alichotumia kudai hati ya mashtaka pamoja na maelezo ya mlalamikaji
sambamba na majeraha aliyopata mtuhumiwa kuwa aliyapata wakati gani na lini.
Kwa upande wake Hakimu Mteite aliiambia
Mahakama kuwa kutokana na ubishani wa pande zote mbili ameona aingilie na
kuwashauri kuwa madai ya upande wa utetezi kuhusu hati ni haki ya kikatiba
kupewa mshtakiwa.
Mteite aliongeza kuwa madai ya majeruhi
ya Mshtakiwa namba mbili ni mbinu za kuchelewesha kesi ambazo mara nyingi
hufanyika ili mahakama ishindwe kuendelea na kesi na kuongeza kuwa yeye binafsi
pamoja na mahakama hakubaliani na suala hilo.
Alisema kama taarifa za ugonjwa huo
zingikuwa za kweli Jeshi la Magereza linajua taratibu ambapo mgonjwa hupelekwa
Hospitali ambapo mahakama ikitambua huhamishia kesi zake hospitali.
Alisema Wakili wa utetezi anapaswa kutambua
kuwa mwenendo wa Mahakama wa siku hizo tofauti na zamani ambapo kesi moja
ilikuwa ikichukua hadi zaidi ya miaka mitatu lakini sasa wamejipanga kumaliza
kesi mapema kabisa.
Kutokana na hali hiyo Hakimu aliahirisha
kesi hiyo hadi Januari 20 Mwaka huu na kumwagiza Wakili wa Utetezi Lwekaza
kuhakikisha inampeleka Mtuhumiwa siku ya kesi kwa njia yoyote hata kama ni
mgonjwa namna gani ikiwa ni pamoja na kumbeba kwa machela au gari la wagonjwa.
Pia alimwagiza mwendesha mashtaka wa
Serikali kuhakikisha anawapatia washtakiwa madai yao ambayo ni kupatiwa hati za
mashtaka, nakala ya maelezo ya mlalamikaji pamoja na mwenendo wa awali wa kesi.
Awali Mwendesha mashtaka wa Serikali
Archiles Mulisa akisaidiwa na Basilius Namkambe alisema washtakiwa wote kwa pamoja
wanatuhumiwa kwa kosa moja la unyang’anyi wa kutumia Silaha kinyume cha Sheria
kifungu cha 287 sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mulisa aliwataja watuhumiwa hao
kuwa ni Mshitakiwa namba moja ambaye ni Askari Polisi PC James mwenye namba
F8302 wa Wilaya ya Mbeya ambaye kabla ya kufikishwa mahakamani alivuliwa
Uaskari baada ya kuhukumiwa kijeshi.
Aliwataja wengine kuwa ni mshtakiwa
namba mbili kuwa ni Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya, Askari
Magereza mwenye namba B 500 Sajenti Juma Mussa(37) wa Gereza la Ruanda
Mbeya,Mbaruku Hamis(29) Mkazi wa Iyela na Amri Kihenya(38) Mkazi wa Iyela.
Akisoma mashtaka yao Mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, Mulisa alisema watuhumiwa hao
walitenda kosa hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo la
Mlima Kawetere barabara ya Mbeya Chunya.
Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja
walitenda kosa hilo kwa kulizuia gari aina ya Pick Up lililokuwa likiendeshwa
na Ezekia Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye alikuwa na mtu
aliyekuwa akifahamika kwa jina la Sreedhar Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia
wakitumia magari madogo mawili ambayo ni GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari
linguine ambalo lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 AINA YA Grand Mark II.
Na mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment