TUNAWE MIKONO MARA KWA MARA |
Baada ya uzinduzi huo hapa mkurugrnzi huyo akinawa mikono kuashiria siku ya unawaji wa mikono duniani |
Makirikiri wa Mbeya wakitumbuiza katika kilele cha kunawa mikono Duniani |
WANANCHI wameaswa kuwa na tabia ya kunawa mikono
kila mara hususani wanapotoka Hospitalini kutibiwa ama kuwatembelea wagonjwa
ili kujikinga na magonjwa ya maambukizi.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa
Sehemu ya Ukaguzi na Uhakiki wa Ubora wa Huduma za Afya kutoka Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk. Henock Ngonyani, alipokuwa mgeni rasmi katika kilele
cha Siku ya Kunawa mikono iliyofanyika katika Hospitaliya Rufaa ya Mbeya.
Dk Ngonyani alisema ni vema mamlaka zinazohusika
kutoa elimu kwa jamii ili kuwa na tabia ya kunawa mikono yao kwa maji safi na
sabuni mara baada ya kutoka kutibiwa au kuwatembelea wagonjwa mawodini ili
kuepuaka magonjwa ya kuambukizwa kama kuhara.
Alisema kama Wizara inajukumu la kuandaa miongozo
ya namna ya kutibi na kujikinga na magonjwa ya kuambukizwa kwa watumishi wa
Afya ambapo tayari Wizara ilikwisha toa miongozo ya Lugha za Kiingereza na
Kiswahili ambayo imeshaanza kutumika.
Aliongeza kuwa zaidi ya Watumishi 10,000 wa
Huduma za Afya katika Hospitali za Mikoa Wilaya na Rufaa nchi nzima wamepewa
mafunzo namna ya kukabiliana na magonjwa ya kuambukizwa wakati wakihudumia
wagonjwa katika Sehemu zao za kazi.
“ Ni matumaini yangu kuwa baada ya kutoa elimu
kwa Watumishi wa Afya nao pia wataweza kuifikia jamii moja kwa moja kwa
kuwaelimisha namna ya kunawa mikono baada ya kutoka Hospitali” alisema
Mkurugenzi huyo.
Aliongeza kuwa Zoezi hilo linakabiliwa na
Changamoto nyingi ambapo ailizitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na ukosefu wa
Vitendea kazi kwa Wahudumu ambapo wao wanatakiwa kujikinga kwanza na magonjwa
ya kuambukizwa kabla ya kutoa huduma kwa mgonjwa.
Alivitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni pamoja na
Gloves na Eploni za kuvaa watoa huduma kabla ya kuanza kumuhudumia mgonjwa ili
asipate magonjwa ya kuambukizwa ambapo aliongeza kuwa upatikanaji wa Vifaa
hivyo umekuwa mgumu kutokana na ufinyu wa Bajeti.
Changamoto nyingine alisema ni kushindwa
kubadilika kwa tabia za baadhi ya Wahudumu kutoka kufanya kazi kwa mazoea na
kwenda kwenye kufuata elimu ya kujikinga na magonjwa ya kuambukizwa kutokana na
elimu waliyoipata.
Aliitaja Changamoto nyingine kuwa ni Uangamizaji
wa taka ngumu zitokanazo na huduma za afya ili kuepukana kabisa na magonjwa ya
kuambukizwa ambapo Hospitali nyingi nchini hazina vifaa hivyo na vilivyopo
havina uwezo wa kuteketeza taka hizo.
Kutokana na changamoto hiyo Dk. Ngonyani alitoa
Wito kwa wadau wa afya kuzipatia msaada Hospitali Nchini wa Vifaa vya
kuteketezea taka ngumu ili kumudu zoezi la kukinga na maambukizi ya magonjwa ya
kuambukizwa ili jamii iweze kuwa safi.
Kwa upande wake Mratibu wa Zoezi la Kunawa mikono
Mkoa wa Mbeya Felister Heller alisema tangu zoezi la kutoa Elimu lianze
kumekuwa na mwitikio mkubwa ambapo tangu Mei Mosi Mwaka huu jumla ya watu zaidi
ya 6000 wamenawa mikono baada ya kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Alisema Elimu hiyo ilianza kutolewa Mwaka 2005
kupitia Magari ya Matangazo ya barabarani(PA) na kupitia kwa wagonjwa
moja kwa moja kabla ya kuanza kupatiwa matibabu ambapo huambiwa umuhimu wa
kunaw mikono baada ya kutoka Hospitalini.
Heller alisema kutokana na mwitikio huo
maambukizi ya magonjwa hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa baada ya wananchi
kuelewa umuhimu wa kunawa ambapo wengi walikuwa wakipata magonjwa ya kuhara na
kipindupindu baada ya kushikana na wagonjwa kisha kula bila kunawa.
Aidha aliishukuru klabu ya Rotary tawi la Mbeya
kupitia kwa Raisi Wake Dk Robert Mbinda kwa msaada walioutoa ambao ni kujenga
sehemu za kunawia wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na tawi lake
katika Hospitali ya Wazazi ya Meta.
Raisi wa Klabu hiyo Dk Mbinda alisema wamejenga
vituo vitatu katika Hospitali hizo mbili kwa gharama ya Shilingi Milioni Tatu
na Laki tano(3,500,000/=)kutokana na michango ya kujitolea ya wanachama wapatao
15.
Picha na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment